March 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge wafunguka kutekwa kwa MO Dewji

Spread the love

BAADHI ya Wabunge hapa nchini wametoa neno kuhusu tukio la kupotea kwa Mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’, huku wakitoa wito kwa serikali kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kutoa taarifa ili kuitoa hofu jamii. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumzia kuhusu tukio hilo lililotokea alfajiri ya leo tarehe 11 Oktoba 2018, katika Gym ya hoteli ya  Colosseum iliyoko Oysterbay jijini  Dar es salaam, Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe amesema serikali ikikaa kimya kuhusu tukio hilo, inaweza kutishia usalama wa nchi ikiwemo uchumi.

Mwambe ameeleza kuwa, kutokana na kuwepo kwa matukio kama hayo, ambayo yalianzia kwa wanasiasa, wanaharakati na watoto kisha mfanyabiashara Mo Dewji,  wafanyabiashara na wawekezaji ndani na nje ya nchi wataogopa kuwekeza hapa nchini.

“Serikali ifanye uchunguzi wa matukio yote na kutoa taarifa kwamba nini kilicho nyuma ya matukio ya kupotea kwa watu. Wasiposema nini kinafanyika na kutoa taarifa, wanaofanya watakuwa wanaendelea sababu watakuwa hawajulikani na kutia hofu kwa wananchi.

Kutokana na hizo ‘trend’ huko nyuma watu wanaona ni kawaida, haijulikana nani atafuata hii inatishia hata uchumi.Sababu wafanyabiashara wakubwa wakisikia mfanyabiashara mwenzao ametekwa hata wafanyabiashara wa kutokea nje wataogopa,” amesema na kuongeza Mwambe.

“Tanzania imekuwa kama fomula (kanuni), kwa sababu matukio kama hayo yalianza kama utani, tumeshuhudia karibuni watoto wakitekwa hakuna juhudi zozote zinazofanyika upande wa serikali na wala kutoa tamko , tumeshuhudia wanasiasa wakifanyiwa tukio kama hilo hilo, akiwemo Lissu alipigwa risasi, Nape katishiwa bastora na mhusika kudaiwa kuwa sio polisi.

baada ya hapo hatukusikia chochote, lakini mpaka sasa uchunguzi wake haujafanyika, wanaharakati kama Roma walishawahi kutekwa hakuna uchunguzi uliofanyika wala taarifa juu ya waliohusika, “ amesema Mwambe.

Naye Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe kupitia akaunti yake ya Twitter amesema aina hiyo ya uhalifu inaota mizizi, huku akitoa wito kwa jamii kutoa taarifa yoyote itakayowezesha kupatikana kwa Mo Dewji.

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia ukurasa wake wa Twitter, amesema anafuatilia kwa karibu suala la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo maarufu.

error: Content is protected !!