WABUNGE wamepitisha azimio la kumchangia fedha aliyekuwa Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule, ili kumfariji kutokana na matatizo ya kiafya aliyoyapata. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Azimio hilo limepitishwa leo tarehe 9 Novemba 2023, baada ya Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, wabunge kumuunga mkono katika uzinduzi wa taasisi yake ya Prof. Jay, aliyoanzisha kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wa figo nchini, unaotarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Baada ya Spika Tulia kutoa wito huo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aidah Kenani, aliliomba mwongozo wa Spika Tulia kuhusu matatizo yaliyomkuta Prof. Jay, huku akipendekeza kila mbunge amchangie fedha kiasi cha Sh. 50,000.
Naye Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku maarufu kama Msukuma, alipendekeza kila mbunge amchangie Prof. Jay kiasi cha Sh. 200,000.
Kutokana na hoja hiyo kuungwa mkono na wabunge wengi, Spika Tulia alitoa mwongozo uliotaka wabunge kumchangia kulingana na uwezo wao kwa muda wa siku mbili, kuanzia leo Alhamisi hadi Ijumaa, kisha zoezi hilo likimalizika Prof. Jay akabidhiwe fedha zilizopatikana.
Kiongozi huyo wa Bunge, amesema pamoja na uzinduzi huo utakaofanyika tarehe 24 Novemba mwaka huu, pia litafanyika zoezi la kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia watu wenye matatizo ya figo.
Awali, Prof. Tulia wakati anaitambulisha taasisi ya Prof. Jay alisema “taasisi hii inatarajiwa kuzinduliwa katika Ukumbi wa Mlimani City, lengo lake pamoja na mambo mengine ni watanzania kuchangisha fedha kusaidia watu wenye changamoto za figo hapa nchini. “
“Mnakaribishwa kwa ajili ya kuungana na Prof. Jay kwenye jambo hili hasa tukizingatia alikuwa mbunge mwenzetu na alipata changamoto hii,” amesema SPika Tulia.
Prof. Jay ameanzisha taasisi hiyo baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi ya figo, ambaye kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kupata matibabu ndani na nje ya nchi.
Leave a comment