August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge wa CCM wapandishwa kizimbani kwa rushwa

Spread the love

WABUNGE watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kudai rushwa, anaandika Faki Sosi.

Waliofikishwa mahakamani leo ni Kangi Lugola (Mwibara) Victor Mwambalaswa (Lupa) na Murad Sadiq (Mvomero).

Maghella Ndimbo, Wakili wa Serikali, aliiambia mahakama, mbele ya Thomas Simba, Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Kisutu, kuwa watuhumiwa hao wanakabiliwa na tuhuma za kupokea rushwa ya Tsh. 30 milioni.

Ndimbo amesema wabunge hao walifanya kitendo hicho tarehe 15 Machi mwaka huu katika Hotel ya Golden Tulip, Dar es Salaam, majira ya saa mbili hadi nne usiku wakiwa kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa.

Anayedaiwa kuombwa rushwa ni Mbwana Magotta, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Gairo.

Amesema washtakiwa waliomba rushwa ili watoe mapendekezo mazuri kuhusu hesabu ya fedha za bajeti ya mwaka 2015/2016 za halmashauri hiyo.

Wote wamekana mashtaka. Wakili amesema uchunguzi bado haujakamilika. Kesi hiyo itatajwa tena 14 April mwaka huu.

Akizungumza na waandishi baada ya kesi kuahirishwa, Lugola amesema mashitaka dhidi yao ya kisiasa, na kwamba ataendelea kutumbua majipu, huku akiiachia mahakama itende haki.

error: Content is protected !!