BUNGE la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), limesikitishwa na mahudhulio duni ya mawaziri wa jumuiya hiyo, jambo ambalo linasababisha baadhi ya hoja kukosa majibu na kukwama kwa baadhi ya miswada. Anaripoti Joseph Ngilisho, kutoka Arusha … (endelea).
Utoro wa mawaziri umesababisha Dk. Abdulah Makame, kuwasilisha hoja binafsi bungeni jana, akitaka Bunge lijadili hoja ya mahudhulio hafifu ya mawazili.
Alisema, “ni bora Bunge hili lijadili kwanza mahudhulio ya mawaziri wa jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sababu utoro wa mawazili bungeni, ulisababisha matatizo makubwa, ikiwamo kuchelewa kupitishwa kwa bajeti ya jumuiya.”
Aliongeza: “Hata leo wakati Bnge linaketi kwa kikao chake, hapakuwa na waziri hata mmoja. Aliyehudhuria ni mwanasheria tu na kuna mawaziri hawajawahi kuhudhulia hata kikao kimoja tangu wachaguliwe.
“Kitendo cha mawaziri kutohudhulia Bunge kinahudhunisha na kufedhehesha na kinaonesha wazi kwamba hawatoi umuhimu kwa shughuli za bunge na jumuiya letu.”
Dk. Makame alisema kutohudhulia kwa mawaziri ni kuonesha dharau kwa Bunge na kuvunja moyo kwa waasisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambao walikuwa na nia ya kutaka mtangamano uendelee katika eneo hili.
Hata hivyo, baada ya kuwasilisha hoja yake na kuungwa mkono na wabunge wengi, Spika wa Bunge hilo alimtaka mtoa hoja, kwenda kuandaa vizuri hoja yake ili aiwasilishe baadaye kwa ajili ya kujadiliwa .
Naye Mashaka Ngole, mbunge kutoka Tanzania ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya sheria, haki na hadhi za wabunge, aliwasilisha ripoti ya marekebisho ya sharia, ili wabunge watoe mapendekezo iwapo kuna haja ya kuzipitia upya na kuzifanyia marekebisho.
Alisema, kanuni nazo zinapaswa kufanyiwa marekebisho ikiwemo kuanzisha kamati mpya za Bunge, ili kuongeza ufanisi, hasa ukizingatia kuwa wanachama wa Jumuiya wameongezeka.
Katika hatua nyingine, bunge hilo limepitisha kwa kauli moja, hoja ya kumpongeza spika wa bunge la Tanzania, Dk. Tulia Akson, kufuatia kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa mabunge duniani (IPU).
Hoja hiyo ililetwa bungeni na Dk. Makame akilishawishi Bunge hilo kumpongeza Spika Tulia kwa kuliletea sifa Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika.
Bunge linaendelea na vikao katika makao makuu ya jumuiya hiyo jijini Arusha.
Leave a comment