August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge Ukawa walaani onevu wa Polisi Z’bar

Spread the love

WABUNGE wa vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi (Ukawa) wamelaani vitendo vya uenevu vinavyofanywa najeshi la Polisi Visiwani Zanzibar, anaandika Faki Sosi.

Vyama vianavyounda ukawa ni pamoja na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), National Legue For Democrasy (NLD) na NCCR-Mageuzi.

Wabunge hao kupitia taarifa waliyoitoa katika vyombo vya habari wamesema kuwa kinachoendelea visiwani humo tangu uchaguzi “haramu” wa marudio Unguja na Pemba, 20 Machi mwaka huu, hali ya kiusalama Visiwani humo imekuwa mbaya.

Wamesema, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayafanya hayo Kwa sababu ya hasira ya kukataliwa na wananchi wengi na kwamba waliona wazi kuwa wananchi wa Zanzibar walikataa kudhulumiwa.

“Tumeshuhudia vikosi vya wanajeshi, Polisi nausalama wa taifa, wakipelekwa kote Unguja na Pemba, kipindi chote cha kuelekea uchaguzi huo ikiwa  mbinu ya kuwatisha raia,

“Hapo ndipo vikosi vya ulinzi na hasa Jeshi la Polisi vimekuwa vikishiriki katika vitendo kadhaa vya ukiukwaji wa haki za raia huko Pemba ambapo kwa zaidi ya miezi miwili sasa, wamekuwa wakipita katika vijiji vyote vya wilaya za Pemba hasa nyakati za usiku,”imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa inaeleza kuwa hatua ya kurudia uchauguzi ule ilitokana na kufutwa kwa uchaguzi  Mkuu wa 25 Oktoba 2015, Maalim Seif Shariff Hamad, aliyekuwa Mgombea urais wa CUF aliyeungwa mkono na UKAWA alishinda. Uchaguzi huo umeelezwa na waangalizi wote wa ndani na nje, kuwa ulikuwa huru na haki.

Inasema kuwa maofisa hao wa vikosi vya usalama wamekuwa wakipiga risasi ovyo, mabomu ya machozi mfululizo, kukamata raia, kuwapiga na kuwatesa; na kisha kuwafungulia mashtaka bandia ambayo hadi leo hii, hakuna yeyote aliyetiwa hatiani.

“Visingizio kadhaa vimetumika dhidi ya raia ikiwa na pamoja kudai kufanywa kwa hujuma kwa taasisi za Serikali na hata mali za watu binafsi. Ukamataji unaofanywa na Polisi haufuati utaratibu wa kisheria unaoeleweka. Tunaamini pia vikosi maarufu kwa uonevu vya Mazombie nao pia hivi sasa wako huko Pemba kuendeleza ubababe huo,”imeeleza.

Taarifa inasema kuwa kuna ushahidi wa watu kuteswa wakiwa mikononi mwa Polisi na hivi sasa kuna watu wanakimbia sehemu wanazoishi wakisakwa na Polisi na wao kuhofia usalama wao. Wakati huu wa mwezi wa mfungo mtukufu wa mwezi wa Ramadhan Polisi wanawashilikisha raia na kuwatia katika majaribu ya kutimiza ibada hiyo.

Wabunge wa Pemba wa Chama cha CUF wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kufuatilia kadhia za wapiga kura wao. Na Wabunge wote wa UKAWA wako pamoja na wenzao katika kipindi hiki kigumu, na UKAWA inatarajia kupeleka timu kamili mara baada ya kikao cha Bunge ili kwenda kuijua hali ya huko kwa undani zaidi.

Vijiji ambavyo vimeathirika na kadhia hiyo huko Pemba ni pamoja na vijiji kadhaa katika majimbo ya Mgogoni, Mtambwe, Wingwi,  Kojani, Kiwani, Ziwani, Tumbe na Chonga.  Vijiji viloathirika kwa ukatili huo ni pamoja na vile vya Mgelema, Kipapo, Kivununi, Mitambuuni, Kinazini, Nanguji na kadhalika.

Watu waliokamatwa na kuachiwa hivi sasa ni 102, waliofunguliwa mashtaka ni zaidi ya 30 na kuna kadhaa ambao wako rumande kesi zao zikiendelea.

Unguja mambo si shwari ambavyo hivi karibuni kutokana na amri ya Dk. Ali Muhammed Shein ya kusafishwa mifugo ndani ya mji wa Zanzibar nguvu kubwa imekuwa ikitumika kutaifisha wanyama hao na risasi za moto kutumika.

Watu 5 wamepigwa risasi na kujeruhiwa vibaya katika kadhia hiyo. Pamoja na kufikishwa Kituo cha Polisi cha Mwanakwerekwe, watu hao hajawapewa  RB Namba katika kile kinachookena Polisi kukwepa kuwajibishwa na matukio hayo.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa nguvu na jeuri ya Polisi kufanya matendo hayo inatokana na Rais wa Jamhuri ya Muunagano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli ambaye ndie Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama.

Umoja huo Hauamini kuwa Dk Magufuli hajui kinachoendelea huko Pemba kwa sababu ni matukio ya muda mrefu sasa, na kama hajui kutakuwa hakuna msamaha maana atakuwa amekoseshwa taarifa na vyombo vyake. Matukio yote ya Unguja na Pemba yamekuwa yakiarifiwa katika vyombo vya habari.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye amekuwa katika Wizara hii kwa miezi 6 sasa ni sehemu ya tatizo linalotokea Pemba  ambapo hata leo katika jawabu yake ya suala la Mhe Yussuf Salim Hussein katika kipindi cha masuala na majibu imedhihirisha tabia yake ya ubabe na kuhusika kwake.

Umoja huo unawataka wananchi wa Unguja na Pemba kuikataa Serikali haramu iliopo madarakani huko Zanzibar kwa njia za amani  na pia wadumishe utaratibu walionao hivi sasa wa kuheshimu sheria na kujizuia kufanya vitendo vya kukinzana na sheria.

 

error: Content is protected !!