Sunday , 2 April 2023
Home Kitengo Habari Kimataifa Wabunge DRC wamuondoa madarakani Spika  
Kimataifa

Wabunge DRC wamuondoa madarakani Spika  

Felix Tshisekedi, Rais wa DR Congo
Spread the love

BUNGE katika Jamhuri ya Demokrasia ya Watu wa Kongo (DRC), limemuondoa madarakani, aliyekuwa Spika wake, Jeanine Mabunda, kufuatia kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye… Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hoja ya kumuondoa kwenye kiti chake Spika Mabunda, iliwasilishwa bungeni na wabunge wa upinzani, ambapo kati ya wabunge 484 waliopo katika Bunge hilo, wabunge 281 waliridhia kiongozi huyo, kuachia ngazi.

Ni wabunge 200 pekee waliopinga uamuzi huo, huku chama cha People’s   Party for Reconstruction and Democracy (PPRD), kilichokuwa kikiongozwa na aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila,  kikiwa ndicho chenye  wabunge wengi bungeni.

Inadaiwa kuwa wabunge walichukua uamuzi huo, baada ya kujiridhisha kuwa Spika wao kuendesha Bunge kwa malengo yake ya kisiasa na kutokuwa muwazi kwenye usimamizi wa fedha za Bunge

Kwa mujibu wa taarifa hizo, pendekezo la kumuondoa mamlakani Spika Mabunda, liliwekwa dhidi yake na wafuasi wa rais wa sasa, Felix Tshisekedi, kwa sababu zizizo nje ya kisiasa.

Hata hivyo, Spika Mabunda amekana tuhuma dhidi yake na amewahi kuomba radhi kufuatia kile alichoita, “hali iliyojitokeza ya kutoelewana” na akalisihi Bunge, kukataa pendekezo hilo.

Kupatikana kwa taarifa kuwa Spika Mabuda ameong’olewa mamlakani, kumekuja katika kipindi ambacho kumeibuka madai kuwa uswahiba kati ya Rais Tshisekedi na mtangulizi wake huyo, umeingia doa.

Tshisekedi ambaye aliingia madarakani kupitia muungano wa chama cha Demokrasia na Maendeleo ya Jamii (UDPS), alidaiwa kuwa na uhusiano wa karibu na Rais Kabila, na kuna taarifa kuwa walitengeneza hata “mwafaka wa kuachia madaraka.”

Hata hivyo, kuondolewa kwa spika huyo wa Kongo kunampa rais Tshisekedi ushindi mkubwa katika harakati zake za kuwania madaraka kati yake na wafuasi wa rais mstaafu, Joseph Kabila.

Aliyekuwa mwanachama wa chama cha Kabila, Justin Bitakwira ameeleza kuwa kilichomsababisha Spika Mabunda kung’olewa madarakani, ni hatua ya Rais Kabila, kupuuza maoni ya wengi.

Bitakwira ambaye amepata kuwa waziri katika serikali ya Rais Kabila anasema, shida iliyopo ni kwamba aliyeteuliwa kuwa spika wa Bunge, hakuwa na uwezo wa kushika nafasi hiyo. Anamtuhumu Rais mstaafu Kabila kwa kuwafikisha hapo.

“Shida ya Rais Kabila, anataka kuumba watu. Kwamba, anaweza kuchukua mtu dhaifu na asiyekuwa na uwezo na kumfanya mtu mkubwa sana. Huyu bwana hakuwa na uwezo wa kushika madaraka aliyopewa,” ameeleza.

Anasema, “tabia hiyo ndiyo inayomgharimu Rais Kabila na ndio utakuwa mwisho wake wa kisiasa yeye na  chama chake.”

Katika uchaguzi mkuu wa tarehe 30 Desemba mwaka 2018, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI), ilimtangaza Rais Tshisekedi kuwa mshindi wa kiti cha urais, nyuma ya mgombea mwingine wa upinzani, Martin Fayulu, pamoja na mgombea aliyekuwa anaungwa mkono na serikali, Emmanuel Shadary.

Mkuu wa CENI, Corneille Nangaa, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema, Bw. Tshisekedi alipata asilimia 38.57 ya kura zilizopigwa.

Fayulu alipinga matokeo hayo na kusema, “…matokeo haya hayana uhusiano hata kidogo na ukweli halisi. Raia wa Congo hawataukubali utapeli kama huu daima.”

Alisema, “Felix Tshisekedi hakupata kura 7 milioni, hakupata. Alizitoa wapi? Haiwezekani. Hii ni kashfa mbaya sana.”

Aliongeza: “Bw Nangaa (mwenyekiti wa CENI) anafuma kitambaa cheusi kwa uzi wa rangi nyeupe. Nangaa na marafiki zake katika FCC (chama tawala), wamekuwa wakichakachua matokeo kumpa ‘kikaragosi’ wao ushindi.”

Hapo awali, Fayulu alikiambia kituo cha redio cha FFI (Radio France International), kwamba matokeo hayo ni “mapinduzi halisi kupitia uchaguzi,” na akatoa wito kwa waangalizi wa uchaguzi kuchapisha matokeo waliyo nayo aliyosema ni ya kweli.

Lakini Tshisekedi kwa upande wake, alimtaja rais aliyekuwa anaondoka Ikulu – Joseph Desire Kanambe Kabila – kama “mshirika muhimu wa kisiasa.”

Kulikuwa na tetesi kwamba, hata kucheleweshwa kwa shughuli ya kutangaza matokeo, kulilenga kutoa muda kwa Rais Kabila na Tshisekedi kuafikiana.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Kimataifa

Marekani yatia mguu maaandamano Kenya, yatoa maagizo kwa Rais Ruto, Odinga

Spread the love  Mabalozi kutoka nchi sita za Magharibi, zikiongozwa na Marekani,...

Kimataifa

Papa Francis alazwa hospitali kutokana na maambukizi ya mapafu

Spread the love  KIONGOZI wa Kanisa katoliki duniani, Papa Francis jana Jumatano...

Kimataifa

Nyumba ya babu yake Makamu wa Rais wa Marekani yatafutwa Zambia

Spread the love  KAMALA Harris, makamu wa rais wa Marekani, amepanga kutembelea...

Kimataifa

Benki ya Uswizi mbioni kuziwekea vikwazo akaunti za siri za Wachina

Spread the love  WAKATI Serikali na Benki ya Uswizi ikichukua hatua kali...

error: Content is protected !!