July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge CUF, wamtega Lipumba

Prof. Ibrahim Lipumba

Spread the love

PROF. Ibrahim Haruna Lipumba, mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), amewekwa njia panda na baadhi ya wabunge wa chama chake hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

“Huyu bwana Lipumba, ameshikwa pabaya na wabunge wake. Ndani ya moyo wake, anapenda kuwafukuza kwenye chama kwa kuwa siyo watiifu kwake,” anaeleza kiongozi mmoja mwandamizi wa chama hicho aliyekaribu na Prof. Lipumba.

Anasema, karibu wabunge wote wa majimbo, hasa wanaotokea Visiwani, ni wafuasi wa Maalim Seif Sharif Hamad, katibu mkuu wa CUF aliyejiondoa kwenye chama hicho, kutokana na madai kuwa Lipumba anatumiwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Anasema, “…lakini analazimika kuwabembeleza, kwa kuwa akiwafukuza tu, atakuwa ameshapoteza ruzuku yote.”

Lipumba aliyesimikwa ndani ya chama hicho na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Katabazi Mutungi, amesababisha CUF kumeguka mapande mawili – moja linaongozwa na yeye na jingine na Maalim.

Tayari baadhi ya wabunge wa chama hicho, majina tunayo, wamejiapiza kufa na Maalim Seif katika kile wanachoita, “ni kumuunga mkono mapambano ya kudai haki.”

Maalim Seif, alitangaza kuondoka CUF juzi Jumatatu kwa kile alichoita, “kupinga hatua ya serikali ya kuungana na Prof. Lipumba kurejesha na kuvuruga harakati za mapambano ya kudai haki.”

Akawataka wafuasi wake na wote wenye mapenzi mema na taifa hili kuunganisha nguvu zao kwa kujiunga na chama cha ACT- Wazalendo. kufuatia

CUF kiliingia kwenye mgogoro uliochochewa na msajili Mutungi, kufuatia Maalim Seif kutoitambua serikali ya Dk. Alli Mohammed Shein.

Mwenyekiti wa wabunge wa CUF, Sulemani Bungara, maarufu kwa jina la Bwege, ameeleza MwanaHALISI ONLINE kuwa yeye na wenzake, wataendelea kubaki kuwa wanachama wa chama hicho.

Naye mbunge mmoja wa CUF ambaye hakupenda kutajwa jina amesema, “nimepata uwakilishi wangu kupitia CUF. Nitaendelea kuwa mwanachama wa chama hiki na hata sasa, niko hapa ninafanya kazi za Bunge.”

Anasema, “sitaondoka CUF, labda hao wanaojiiita wenye chama, wanifukuze. Nitabaki ndani ya chama hiki na nitaendelea kuwahudumia wananchi wangu.”

Alipoulizwa iwapo atamfuta Maalim Seif baada ya kumaliza ubunge wake, mbunge huyo amesema, “hakuna shaka. Mimi ni mfuasi wa Maalim na kwamba ninachosubiri sasa, ni kumaliza ubunge wangu, ili niuungane naye katika safari ya mabadiliko.”

error: Content is protected !!