October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge Chadema wasalitiana

Spread the love

SIRI imefichuka. Baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walikaidi chini kwa chini, maelekezo ya mwenyekiti wao, Freeman Mbowe. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Taarifa kutoka mjini Dodoma zinasema, pamoja na tangazo la Mbowe, kutaka wabunge wake wote kutoingia bungeni, bado baadhi ya wale walionekana kutii maelekezo hayo, “nao walisaliti wenzao.”

Mbowe alitangaza wiki iliyopita, kuwa wabunge wote wa Chadema, ni mwiko kuhudhuria mkutano wa Bunge la Bajeti, Kamati za Bunge na kukaribia viwanja vya Bunge.

Alisema, maamuzi hayo yamechukuliwa ili kuweza wabunge hao, kujikinga na maambukizi ya gonjwa hatari la Corona.

Alisema, “wabunge wote wa Chadema, hawaruhusiwi kufika kabisa katika eneo lote la Bunge, Dodoma na Dar es Salaam. Badala yake, Mbowe akaelekeza wajiweke karantini kwa wiki muda wa angalau wiki mbili.”

Kwa mujibu wa taarifa ya Bunge iliyosambazwa kwa vyombo vya habari jana Jumatano, ni wabunge 15 tu, kati ya wabunge 45 wa Chadema, ndio walionekana kuwa “walikomaa mpaka mwisho.”

Spika wa Bunge, Job Ndugai, alieleza juzi Jumanne, kwamba wabunge wote ambao hawajaingia bungeni kuanzia tarehe 1 Mei mwaka huu, wanapaswa kurejesha kiasi cha Sh. 2 milioni walizolipwa.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee akitafakari jambo bungeni

Sharti jingine walilopewa, ni kurejea bungeni, wakiwa na ni cheti cha daktari kinachothibitisha kuwa hawana maambukizi ya Corona.

Wabunge ambao wameweza kukwepa rungu la Spika, ni pamoja na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema; mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka, Mbunge wa Arumeru Magharibi, Gibson Meiseyeki na Suzan Kiwanga, Mbunge wa Mlimba.

Wengine waliomo kwenye orodha hiyo, ni wabunge wa Viti Maalum, Suzana Lyimo, Lucy Owenya, Jesca Kishoa, Yosepher Komba, Esther Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, Salome Makamba, Grace Tendega, Kunti Yusuf, Cecilia Paresso, Ruth Mollel na Sophia Mwakagenda.

Pia wamo, Hawa Mwaifunga, Anatropia Theonest, Conchester Rwamlaza, Gimbi Masaba, Sasana Mgonokulima, Zubeda Sakuru, Mary Muro, Sabreena Sungura, Tunza Malapo na Risala Kabongo ambao wote ni wa viti maalum.

Kupatikana kwa habari kuwa baadhi ya wabunge wamejitenga na wenzao, kumekuja wiki moja baada ya Willifred Lwakatare, kuwatuhumu baadhi ya wabunge wa Chadema kugeuka “wanafiki.”

Lwakatare alisema, baadhi ya wabunge wa Chadema wamekuwa wakiingia bungeni huku wakiwa wamevaa mabaibui; na kujifunika nguo mwili mzima ili kutotambulika.

Aidha, kupatikana kwa habari hizi kumekuja siku tatu baada ya chama hicho, kutangaza kuwafuta uwanachama wabunge wake wanne.

Wabunge waliovuliwa uwanachama, ni Anthony Komu, mbunge wa Moshi Vijijini; Willifred Lwakatare, mbunge wa Bukoba Mjini; Joseph Selasini, mbunge wa Rombo na mbunge wa Momba, David Silinde.

Vilevile, kupatikana kwa habari hizi kumekuja wiki mbili baada ya wabunge takribani 15, kugoma kuondoka bungeni na hivyo kutakiwa kujieleza.

Wabunge waliopewa barua za kujieleza kwa nini wasivuliwe uwanachama wa chama hicho, ni pamoja na Peter Lijualikali (Kilombero); Latifa Chande, Mariam Msabaha, Rose Kamili Slaa na Risala Kaboyonga.

Katika orodha hiyo, wamo pia Mbunge wa Moshi Mjini, Jafari Michael; Mbunge wa Karatu, Willy Qambaro; Bukoba Mjini na Mbunge wa Viti Maalum Sabrina Sungura.

Akizungumzia mgawanyiko uliyopo kwenye kundi la wabunge wa Chadema, mmoja wa wafanyakazi wa Bunge amesema, “hapa imethibitika kuwa Chadema kimepasuka.”

Amesema, “kuna ambao wamerejesha fedha. Kuna ambao hawakuwa wamelipwa fedha na wapo ambao hawakuingia bungeni, lakini wakiwa na ruhusa ya Spika. Hivyo siyo jambo zuri kueleza jambo, wakati hujalifanyia kazi.”

Hata hivyo, Selasini anasema, ni muhimu Spika Ndugai akaweka wazi jambo hili.

Amesema, “ni lazima ijulikane, nani amerejesha fedha; nani hakuchukua, nani alikuwa anaingia bungeni na nani alikuwa na ruhusa ya Spika.

Anasema, “jambo hili lisipowekwa sawa, itakuwa kashfa kubwa kwa Bunge lenyewe. Iweke orodha ya walioingia bungeni, waliolipa kadri ya maagizo ya Spika, wenye ruhusa; waliobaki watajulikana. Ni muhimu sana. Hili ni suala la uadilifu.”

error: Content is protected !!