July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge 5 CUF wabanwa mbavu Handeni

Sonia Magogo,Mbunge wa CUF Viti Maalum Tanga

Spread the love

WABUNGE watano kutoka Chama cha Wananchi (CUF), tarehe 3 Agosti 2019 walikamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi wilayani Handeni, Tanga kwa madai ya kufanya mkutano bila kibali. Anaandika Danson Kaijage, aliyepo Handeni…(endelea). 

Wabunge hao ni Mussa Mbaruku, Tanga mjini; Zainabu Mndolwa, Viti Maalum Dar es Salaam; Rukia Kassim, Pemba; Rehema Migila, Tabora na Sonia Magogo, Tanga.

Masoud Mhina, Naibu Mkurugenzi wa Mafunzo, Udhibiti na Itifaki Taifa kwenye chama hicho amesema, wabunge hao walihojiwa kwa zaidi ya sita jana.

Amesema, walihojiwa kwa madai ya kuitisha mkusanyiko isivyo halali, kuwakataza wananchi wasiwekewe namba kwenye nyumba zao na kukataza wananchi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

“Walituachia ila tumeambiwa mimi na wabunge wangu wote turipoti tena kituoni hapo tarehe 7 Agosti,” amesema Masoud.

Edward Bukombe, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga amesema, waliwakamatwa wabunge hao kwasababu waliingia kwenye Jimbo la Handeni mjini bila kuwa na kibali cha kufanya mikutano.

Amesema, mwongozo uliopo ni kuwa kila mbunge anatakiwa kufanya mkutano kwenye jimbo lake na sio sehemu nyingine.

“Sababu ni kwamba, walikuwa wanafanya shughuli za mikutano bila kibali, na lile eneo sio la kwao, wanatoka maeneo mengine. Ingekuwa wao ni wabunge wa eneo hilo, hapo ingekuwa sawa,” amesema Bukombe.

Awadhi Chanyendo, mwenyekiti wa chama hicho katika Wilaya ya Handeni amesema, waliomba kibali kwa ajili ya ufunguzi wa matawi pamoja na kikao cha wananchi wa Kata ya Mabanda lakini hawakujibiwa.

error: Content is protected !!