January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge 37 wapitisha muswada bungeni

Bunge likiwa halina wabunge wa kutosha

Spread the love

KATIKA hali inayoonesha wabunge wengi kuwa na homa ya uchaguzi, jana ni wabunge 37 pekee kati ya 354 ndio waliopitisha Mswada wa Sheria ya Masoko ya Bidhaa ya Mwaka 2015. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Katika idadi hiyo ya wabunge, ni mawaziri na manaibu waziri wanne tu waliokuwepo bungeni wakati wa muswada huo.

Mbali na wabunge kutokuwepo bungeni, uchangiaji katika muswada huo ulionekana kupitishwa kirahisi jambo ambalo linatia mashaka kama wabunge wameusoma kweli mswada huo au la!

Jambo lingine ambalo limeonesha kuwa wabunge wamechoka kuendelea na vikao vya bunge ni pale ambapo bunge la jioni lilipoanza saa 10:00 kama ilivyo kawaida na kumalisha shughuli zake saa 10: 57 badala ya saa 12:00 jioni.

Pamoja na hali ambayo inaonesha wazi kuwa wabunge ni watoro na hawafanyi kazi yao ipasavyo, jana bunge lilipitisha muswada huo.

Pamoja na uchache huo, walioonekana kuchangia ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalum, Martha Mlata (CCM) ambaye alipongeza kuletwa kwa sheria hiyo huku akisema kuwa imechelewa.

Mlata ameshauri kuwepo kwa mfumo mzuri ambao utawawezesha wakulima wa vijijini kujua bei gani ipo katika soko kwa wakati huo ili wasipitwe na kuweza kwenda na wakati.

Amesema, ni lazima sheria hiyo iwasaidie kutofautisha ubora wa bidhaa, ziwe na nembo inayotambulisha bidhaa inapotokea na ubora wake pamoja na kutofautisha bei kulingana na ubora wa bidhaa.

“Sheria hiyo inatakiwa kutambua mazao yote bila kubagua aina ya zao na kuhakikisha mapato yanayopatikana katika masoko kutokana na uuzaji wa bidhaa yanarudi kuwanufaisha wananchi.” Amesema.  

Mbunge wa Mkanyegeni, Mhandisi Habibu Mnyaa (CUF) amesema, ana wasiwasi kama nchi ipo tayari kwa muswada huo kwa wakati huu.

Amesema, Tanzania haina mashaka katika kupitisha sheria na kuweka mipango mizuri tatizo ni kwamba, utekelezaji wake umekuwa mgumu.

Aidha ametaka kujua ni kwa kiasi gani Zanzibar wameshirikishwa ama wana ufahamu kiasi gani muswada huo.

Mbunge wa Longido, Lekule Laizer (CCM) ameshauri kuwekwa kwa mazingira mazuri ya miundombinu na bidhaa katika masoko.

Amesema, wakulima hivi sasa wananyanyasika, wanatumia gharama kubwa katika uzalishaji ambazo hazirudi baada ya kufika kwenye masoko.

Akiwasilisha bungeni muswada huo, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima amesema, muswada huo umegawanyika katika sehemu kuu 18.

Malima amesema, sehemu ya kwanza kama ilivyorekebishwa ina vifungu 1, 2, 3 ambavyo vinahusu masuala ya utangulizi ambayo yanajumuisha jina la sheria, tafsiri ya maneno na matumizi ya sheria hiyo.

 Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara kuhusu muswada huo, Makumu Mwenyekiti na Mbunge wa Mkinga, Danstan Kitandula (CCM) amesema, kamati inashauri sheria hiyo ifungue mlango wa mamlaka kushirikiana na Taasisi za Serikali.

Ni wakati wa kutengeneza kanuni kuhusu bidhaa husika kabla ya binafsi zinazotaka kutumia sheria ya masoko ya bidhaa zinaweza kusajiliwa na Soko la Bidhaa.

Aidha kamati inashauri, leseni ya Soko (Sehemu II) kuwepo kwa kipengele kwenye sheria ambapo mamlaka itaruhusu kutolewa kwa leseni za muda mfupi kwa watendaji wa soko la bidhaa.

“Kwa kuwa leseni za muda mfupi zitasaidia pamoja na mambo mengine kukidhi masharti ya soko la utendaji kazi kabla ya kupatiwa leseni ya kudumu,” amesema Kitandula.

Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika Wizara ya Fedha, David Silinde (Chadema) akisoma maoni ya kambi hiyo amesema, kambi inaungana na wadau ambao wameliona tatizo la kuziweka pembeni mamlaka na wakala za serikali.

Amesema, kuna bidhaa ambazo zinatakiwa ziingie katika mfumo mzima au mnyororo wa uongezwaji wa thamani kabla ya kuwekwa katika soko la bidhaa.

error: Content is protected !!