Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wabunge 36 waanguka kura za maoni CCM
Habari za SiasaTangulizi

Wabunge 36 waanguka kura za maoni CCM

Spread the love

TAKRIBANI wabunge 36 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), nchini Tanzania, wameanza vibaya safari yao ya kutetea nafasi zao, katika uchaguzi mkuu wa 28 Oktoba mwaka huu. Anaripoti Regina Mkonde …(endelea)

Kura za maoni ndani ya chama hicho zimefanya kwa siku mbili juzi Jumatatu, tarehe 20 Julai na jana Jumanne.

Kwa mujibu wa rekodi zilizochukuliwa na MwanaHALISI, wabunge wote hao, wameshindwa katika hatua ya kwanza ya kura za maoni, jambo linawaweka pagumu kupitishwa kugombea tena nafasi hizo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa katiba ya CCM, kura ya maoni, zinachukuliwa kama mapendelezo ya awali, ingawa matokeo yake, hupewa uzito mkubwa wakati wa kufanya maamuzi.

Soma zaidi hapa

Ngeleja, Bukwimba, Maige na Kalanga wapigwa

Miongoni mwa wabunge walioshindwa katika hatua hiyo ya awali, ni pamoja na aliyekuwa mbunge wa Babati Vijijini, mkoani Manyara, Jitu Soni; aliyekuwa mbunge wa Mufindi Kusini, mkoani Iringa, Medard Kigola na mwenzake wa Kilolo, Venance Mwamoto.

Wengine walioangukia pua, ni aliyekuwa mbunge wa Kyera, mkoani Mbeya, Dk. Harrison Mwakyembe; aliyekuwa mbunge wa Babati Mjini, mkoani Manyara, Pauline Gekul; aliyekuwa mbunge wa Serengeti, mkoani Mara, Mwalimu Chacha Marwa Ryoba; aliyekuwa mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba na Balozi Diodorus Kamala, aliyekuwa mbunge wa Nkenge.

Dk. Mwakyembe na Mgumba, ni mawaziri katika serikali ya Rais John Pombe Magufuli. Wakati Dk. Mwakyembe akiwa waziri kamili wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mgumba ni naibu waziri wa kilimo.

Katika orodha hiyo ya walioshindwa kura za maoni, wamo pia, aliyekuwa mbunge wa Ileje, mkoani Songwe, Janeth Mbene; aliyekuwa mbunge wa Mwanga, mkoani Kilimanjaro, Prof. Jumanne Maghembe; aliyekuwa mbunge wa Ndanda, wilayani Masasi, mkoani Mtwara, Cecil Mwambe; aliyekuwa mbunge wa Misungwi, mkoani Mwanza, Charles Kitwanga na aliyekuwa mbunge wa Kasulu Mjini, mkoani Kigoma, Daniel Nswanzugwako.

Prof. Maghembe, Kitwanga, waliwahi kuhudumu kwenye nafasi ya uwaziri, ndani ya serikali ya Rais Magufuli. Kila mmoja aliondolewa kwa wakati wake.

Wengine walioshindwa kura za maoni, ni Selemani Sadiq Murad, aliyekuwa mbunge wa Mvomero, Peter Lijualikali, aliyekuwa mbunge wa Kilombero, Goodluck Mlinga, aliyekuwa mbunge wa Ulanga, wote wakitokea mkoa wa Morogoro.

wengine, ni Dk. Shukuru Kawambwa, aliyekuwa mbunge wa Bagamoyo, mkoani Pwani, Albert Obama, aliyekuwa mbunge wa Buhigwe, mkoani Kigoma na Godfrey Mgimwa, aliyekuwa mbunge wa Kalenga, mkoani Iringa.

Katika orodha ya hiyo ya waliopuputishwa kwenye kura za maoni, wamo pia, aliyekuwa mbunge wa Temeke, jijini Dar es Salaam, Abdallah Mtolea; aliyekuwa mbunge wa Liawale, mkoani Lindi, Zuberi Kuchauka; aliyekuwa mbunge wa Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Maulid Mtulia; aliyekuwa mbunge wa Sengerema, mkoani Mwanza, William Ngeleja; aliyekuwa mbunge wa Simanjiro, mkoani Arusha, James Millya na Julius Kalanga aliyekuwa mbunge wa Monduli, mkoani Arusha.

Mtolea, Pauline Gekul, Ryoba, Kuchauka, Mwambe, Mtulia, Milya, Lijualikali na Kalanga, walikuwa miongoni mwa wabunge na madiwani kadhaa wa upinzani nchini Tanzania, waliovihama vyao vilivyowapata kugombea nafasi hizo za ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kujiunga na CCM.

Mtulia aliangushwa na Abbas Tarimba; Mwambe ameangushwa na Oscar Ng’itu, Kalanga ameangushwa na Fredirck Lowassa, mtoto wa waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa; huku Milya, Mtolea na Lijualikali, wakiangushwa na watu ambao waliwaangusha wao kwenye kinyang’anyiro hicho wakati walipogombea kupitia upinzani – Christopher ole-Sendeka (Simanjiro), Abass Mtevu (Temeke) na Abubakary Asenga (Kilombero).

Mwambe ameshika nafasi ya tatu katika kinyang’anyiro hicho, baada ya kupata kura 33, huku Ng’itu “akijichotea kura 250” na Faraja Nandala, akishika nafasi ya pili kwa kupata kura 154.

Karibu wabunge wote waliondoka upinzani na kukimbilia chama tawala, waliimba kwa sauti kubwa, kile kilichoitwa, “kuunga mkono juhudi za rais.”

Wengine waliotangazwa kushindwa kura za maoni, ni aliyekuwa mbunge wa Msalala, mkoani Shinyanga, Ezekiel Maige; aliyekuwa mbunge wa Busanda, mkoani Mwanza, Lolencia Bukwimba; aliyekuwa mbunge Handeni Mjini, mkoani Tanga, Omari Kigoda; aliyekuwa mbunge wa Hanang, mkoani Manyara, Dk. Mary Nagu na aliyekuwa mbunge wa Chemba, mkoani Dodoma, Juma Nkamia.

Wapo pia, Prof. Norman Sigalla, aliyekuwa mbunge wa Makete, mkoani Iringa;

Mbaraka Bawazir, aliyekuwa mbunge wa Kilosa, mkoani Morogoro; Jorum Hongoli Lupembe, aliyekuwa mbunge wa Njombe; Mboni Mahita, aliyekuwa mbunge wa Handeni Vijijini, mkoani Tanga, Ally Ungando, aliyekuwa mbunge wa Kibiti, mkoani Pwani; aliyekuwa mbunge wa Kiembesamaki, Visiwani Zanzibar, Ibrahim Raza na Mbaraka Dau, aliyekuwa mbunge wa Mafia, mkoani Pwani.

Kuangushwa kwa vigogo hao, wakiwamo wateule wa rais na waliotoka upinzani, kunakiweka CCM katika mazingira magumu, katika kufanya maamuzi ya kuwarejesha ama kuwatosa.

Soma zaidi hapa

Waliounga mkono juhudi, wabunge na wateule waanguka kura za maoni

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Mwakyembe : Zanzibar waliongoza kutaka Serikali 2 za muungano

Spread the love  MWANASIASA mkongwe nchini, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema mjadala wa...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

error: Content is protected !!