Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wabunge 10 Chadema wamgomea Mbowe, watinga bungeni
Habari za SiasaTangulizi

Wabunge 10 Chadema wamgomea Mbowe, watinga bungeni

Bunge la Tanzania
Spread the love

TAKRIBANI wabunge 10 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamegoma kutii maelekezo yaliyotolewa na mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Taarifa kutoka bungeni mjini Dodoma zinasema, wabunge kadhaa wa chama hicho, wakiongozwa na David Silinde, wamepinga maagizo ya Mbowe na kuamua hudhuria mkutano wa Bunge.

Silinde ambaye ni katibu wa wabunge wa Chadema, amewaambia waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, “sikubaliani na maelekezo ya mwenyekiti wangu, yanayoelekeza sisi wabunge wake, kutoingia bungeni.”

“Nimekuja hapa kuwakilisha wananchi wangu wa Momba, ambao baadhi yao wanakufa kwa magonjwa mbalimbali, ikiwamo ugonjwa huu wa Corona. Hivyo basi, nimeona siyo busara mimi kuwa nje, wakati wananchi wangu wanakufa,” ameeleza.

Jumamosi iliyopita, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni (KUB), aliagiza wabunge wa chama chake, kutoingia bungeni kwa kile alichoita, “kujikinga na maambukizi ya Corona.”

Katika maelezo yake, Mbowe aliwataka wabunge wa Chadema kutokanyaga katika viwanja vya Bunge, pamoja na kukwepa kurudi majimboni mwao hadi watakapotihibitika kwamba hawana maambukizi ya ugonjwa huo.

Alisema, “wabunge wa Chadema waache mara moja kuhudhuria vikao vya bunge na kamati za Bunge. Wabunge wote wa Chadema kutokufika kabisa katika eneo lote la Bunge, Dodoma na Dar es Salaam. Wajiweke katika karantini kwa muda usiopungua wiki mbili.”

Mbowe ameutaka uongozi wa Bunge kusitisha shughuli za mhimili huo kwa muda wa siku 21, ili kuruhusu wabunge na watumishi wa Bunge kwenda karantini, kuwapima na familia zao, kwa lengo la kubaini watu walioambukizwa ugonjwa huo.

Amesema, hatua hizo zimechukuliwa kufuatia maambukizi ya ugonjwa huo kuongezeka.

Wabunge wengine wa Chadema waliongia bungeni, ni pamoja na mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali; mbunge wa Rombo, Joseph Selasini; mbunge wa Viti Maalum, Ratifa Chande; mbunge wa Moshi Vijijini, Antony Komu na Sabrina Sungura, mbunge wa Viti Maalum, kutokea mkoa wa Kigoma.

David Silinde, Mbunge wa Momba (kushoto). Kulia ni Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini

Wabunge wangine wa Chadema walioingia bungeni na kukaidi amri ya mwenyekiti wao, ni Suzan Masele, Mbunge wa Viti Maalum Mwanza, Jafary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini, Antony Komu, Mbunge wa Moshi Vijijini na Mariam Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum Zanzibar.

Akichangia mjadala kuhusu wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Silinde ameliambia Bunge kuwa wabunge wote wanatakiwa kupambana hadi mwisho katika janga hilo, ili kuhakikisha wananchi wanarejea katika hali zao za kawaida.

Silinde amesema kwa sasa wananchi hawatakiwi kumlaumu mtu au chama chochote cha siasa juu ya uwajibikaji kuhusu suala hilo, kwa kuwa janga hilo linahitaji uwajibikaji wa kila mtu.

Jafary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini

Amesema: “Najua Corona ni janga la kimataifa ambalo linahitaji uwajibikaji, sio janga la mtu mmoja au chama cha siasa, ni la kwetu sote.  Corona ni janga, dunia inalia, na sisi Watanzania hatupaswi kulia bali ni kupambana ili kusaidia wananchi wetu waweze kutoka nje.”

Ameongeza: “Na huo ndio wajibu wetu wa kibunge, wajibu wa kibunge ni kupambana hadi mwisho, hilo nimeona niliseme.”

Amesema, amuamua kuhudhuria vikao vya Bunge ili kuwasilisha malalamiko ya wananchi wa jimbo lake, ikiwemo changamoto ya miundombinu mibovu ya barabara.

“Wizara ya ujenzi ni kiungo kikuu cha uchumi katika nchi yetu, wananchi wa Momba wamenituma kusema haya na ninasema kwa niaba yao. Katika Halmashauri ya Momba, barabara zilizochini ya TARULA hazipitiki. Nikaona nikishindwa kusema hilo, nitashindwa kupeleka mrejesho kwa wananchi wangu wa Momba,” amesema Silinde.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!