July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Waathirika mafuriko wapaza sauti serikalini

Spread the love

WAATHIRIKA wa mafuriko yaliyotokea katika vijiji vya Tindiga A, B, Maluwi, Mambegwa na Changarawe wilayani Kilosa, Morogoro wameiomba serikali kuwapatia mbegu zaidi ya tani 20 za muda mfupi ili ziweze kuwasaidia katika kilimo, anaandika Christina Haule.

Wananchi hao waliopatwa na mafuriko yaliyosababisha watu 6800 kupoteza makazi, vyakula huku mazao yao kuharibiwa walitoa ombi hilo kwa wati tofauti mbele ya waandishi wa habari.

Tindiga Likungulu, mwenyekiti wa kijiji hicho amesema kuwa, baada ya kutokea mafuriko hayo, kusababisha wananchi nyumba zao, mashamba kuharibiwa na mafuriko pamoja na mali nyingine iliwalazimu kuhama katika makazi hayo na kutafuta hifadhi kwenye maeneo yaliyotengwa na serikali.

Batista Chang’a, Mtendaji wa Kijiji cha Tindiga amesema, katika kijiji hicho pekee wananchi walioathiriwa na mafuriko hayo ni 3,600 na kwamba wanakabiliwa na tatizo la upungufu chakula, maji safi na salama pamoja na mbegu.

Maximilian Ndwangira, Ofisa Maafa Wilaya ya Kilosa amesema, Serikali ya Wilaya ya Kilosa inatarajia kutoa viwanja 240 kwenye maeneo salama na kwamba, zinahitajika Sh. 84 milioni kwa ajili ya gharama za upimaji viwanja hivyo.

Amesema kuwa, ni kweli wananchi hao waliathiriwa na mafuriko hayo na wanahitaji mbegu kwa ajili kupanda kwenye mashamba yao na tayari ombi hilo limewasilishwa kwa uongozi wa Serikali ya Wilaya.

John Henjewele, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa amesema, serikali inaangalia namna ya kuweza kuwasaidia wakazi hao waliopatwa na mafuriko katika vijiji hivyo ikiwemo Mbegu.

Lusako Mwakiluma, Mkurugenzi wa Taasisi ya Wezesha Trust Fund ya Morogoro iliyokabidhi misaada mbalimbali kwa wananchi hao amesema, msaada huo ni kwa ajili ya kuwapunguzia makali ya maisha wananchi hao.

error: Content is protected !!