December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Waarabu wamwaga bilioni 16 – Zanzibar, watoa ajira 400

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi

Spread the love

 

ZAIDI ya ajira 400 zinatarajiwa kutolewa baada ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) kutia saini mkataba wa ushirikiano kati yake na Shirika la Ndege la Dubai Air Travel Agency (Dnata) litakalohusika kutoa huduma mbalimbali kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Visiwani humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Pia kampuni hiyo ya Dnata inayofanya shughuli zake katika viwanja vya ndege 126 kwenye nchi mbalimbali duniani, pia imethibitisha kuwekeza Dola za Marekani milioni saba sawa na Sh bilioni 16.1 kutekeleza mradi huo Visiwani humo.

Hayo yameelezwa leo tarehe 24 Novemba, 2021 Visiwani Zanzibar na Ofisa Mtendaji wa kampuni ya Dnata, Steve Allen katika hafla ya utiaji saini mikataba minne inayohusu uendeshaji wa huduma katika Uwanja wa Abeid Amani Karume.

Dnata ambayo ni kampuni yenye makao makuu katika Falme za Kiarabu – Dubai inatarajiwa kutoa huduma za abiria na mizigo, uendeshaji, huduma ya kumbi za wageni zilizo katika uwanja huo wa ndege, huduma za maduka na mikahawa.

Katika utoaji wa huduma hizo, Dnata itasimamia pia kampuni nyingine za Egis Airports Group, Emirate leisure retail kutekeleza majukumu hayo kikamilifu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema mikataba imetiwa saini kwa madhumuni ya kuboresha huduma hizo katika uwanja wa ndege.

Amesema Serikali imeamua kutafuta makampuni yenye sifa duniani kuja kushirikiana katika uendeshaji wa kiwanja hicho cha ndege kwa madhumuni ya kutoa huduma bora na za kiwango cha kimataifa.

“Serikali imewekeza fedha nyingi kiasi cha Dola za Marekani milioni 128 katika ujenzi wa jengo la Terminal 3, pia tumeimarisha miundombinu ya barabara, uzio pamoja na maegesho ya magari hivyo tumeona ni busara kutafuta kampuni za kimataifa zitoe huduma zinazofanana na hadhi ya jengo letu jipya la Terminal 3.

“Kampuni tulizozipata baada ya mchakato uliochukua muda mrefu uliotokana na majadiliano mengi yaliyokuwa na dhamira ya kulinda masilahi ya nchi, nafurahi kusema ni kampuni kubwa duniani zenye sifa, uwezo na uzoefu mkubwa unaokubalika na kuaminika kimataifa,” amesema.

Rais Dk. Mwinyi amesema Kampuni hizo ni kampuni ambazo zina shughuli zake katika nchi nyingi duniani, hivyo Zanzibar itapata huduma nzuri.

“Kampuni ya Dnata inafahamika kwa uwezo na uzoefu wake mkubwa katika uendeshaji wa viwanja vya ndege, imeanzishwa tangu mwaka 1959 na imekuwa ikiendesha shughuli zake katika viwanja vya ndege 126 katika nchi mbalimbali duniani.

“Ina uzoefu mkubwa katika masuala ya kutoa huduma za abiria, ushughulikiaji wa mizigo, kuweka taratibu nzuri na mwenendo wa ndege na masuala mbalimbali ya usalama wa abiria mizigo na miundombinu ya viwanja vya ndege,” amesema.

Aidha, amesema maamuzi ya kushirikiana nao yamelenga kuimarisha uchumi kwa mtazamo mpana.

“Dhamira yetu ni kuona tunainua idadi ya mashirika ya ndege yanayofanya safari zake hapa Zanzibar, ongezeko la ndege litaambatana na ongezeko la watalii, wageni, mizigo na ukuaji wa biashara pamoja na soko la ajira,” amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Rahma Kassim Ali amesema wizara ilifanya uchambuzi wa kina pamoja na timu ya majadiliano ilikubaliana kuwa kampuni ya Dnata yenye makao yake Dubai ina sifa zote.

Amesema wizara itatoa ushirikiano wa kutosha kwa kampuni hiyo ili ifanye kazi kwa ufanisi na kutimiza malengo ambayo serikali imejiwekea.

error: Content is protected !!