June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vyombo vya habari vyatathminiwa

Spread the love

VYOMBO vya habari hasa vile vinavyoendeshwa kwa kutumia kodi za Watanzania vimetakiwa kutoa habari bila ya upendeleo hasa zinazojenga na sio kuliingiza taifa katika machafuko. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa amesema taarifa ya mtandao huo kuhusu ufuatiliaji wa awali wa mwenendo wa vyombo vya habari katika kuripoti habari za uchaguzi tangu kampeni zilipoanza 22 Agosti, 2015 hauridhishi.

Olengurumwa amevitaja vyombo vya habari vya umma kuwa vinaripoti kampeni za uchaguzi kwa kupendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku vikitoa nafasi ndogo kwa vyama vya upinzani na wakati mwingine kuvipuuza kabisa.

Pale vyombo hivyo vinaporipoti habari zinazohusu vyama au wagombea wa upinzani, mara nyingi huwa ni zile zinazowachafua.

“Magazeti ya umma kama vile Habari Leo na Daily News yanaonesha wazi kupendelea chama tawala kwa kukipa nafasi kubwa ya mbele, huku vyama vingine vikipewa nafasi ndogo au taarifa zenye mrengo hasi.

“Mfano Mgombea Urais wa CCM, John Magufuli alipokuwa Tabora mkutano wake ulirushwa moja kwa moja na TBC pamoja na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alipokuwa mkoani Kagera kumnadi mgombea huyo.

“Vyombo vya habari vya umma ivikumbukwe kuwa chombo cha habari hasa vyombo vinavyoendeshwa na kodi za wananchi vinatakiwa kutoa fursa sawa kwa vyama vyote,” amesema Onesmo.

Aidha, Olengurumwa amesema kinyume na ilivyotarajiwa, vyombo vya habari binafsi ndivyo vinaonekana vya umma kwa kutoa habari kwa kuzingatia usawa kwa vyama na wagombea tofauti.

Amevitaja vyombo vilivyo chini ya IPP Media, AZAM Media na Mwananchi Communication Ltd vilivyoonekana kutoa fursa sawa kwa vyama badala ya kupendelea chama tawala, vyama vikubwa au vidogo.

Amesema tofauti na gazeti la Uhuru linalomilikiwa na CCM, gazeti la Tanzania Daima na stesheni ya televisheni ya Star TV vinajitahidi kutoa taarifa kama zinavyotolewa na wagombea na wapambe wao.

Akizungumzia usalama kwa wanahabari, Olengurumwa amesema wamegundua jinsi vyombo vya habari vinavyoshindwa kutoa fursa sawa kipindi cha uchaguzi ndivyo wanavyozidi kujiweka kwenye mazingira hatarishi.

Mbali na changamoto hiyo amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kulinda usalama wa wanahabari kwa kutambua mchango wao muhimu kwa jamii wa kuelimisha na kuhamasisha uwajibikaji kwa masuala ya nchi yao.

“Tarehe 25 Julai, 2015 tulipokea malalamiko ya kufungiwa kwa Radio ya jamii ya “Radio Kyela” ya mkoani Mbeya inasemekana ni kwa sababu za kisiasa. Tarehe 31 Julai, 2015 mwandishi Benson Mwakalinga aliyeko Kyela, mkoani Mbeya, alipigwa na viongozi wa CCM.

“Tarehe 17 Agosti 2015 waandishi wa habari wanne walivamiwa na kupigwa wakiwa kazini na 11 Septemba, 2015 mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru, Christopher Lissa alipigwa na wafuasi wa UKAWA waliodai kuwa katumwa na CCM,” amesema Olengurumwa.

THRDC itatoa majaketi 200 kwa klabu 10 za waandishi wa habari Tanzania, ambayo waandishi watayatumia wakati huu wa uchaguzi kwa lengo la kusaidia kuwakinga na vurugu kwa kutambuliwa kuwa wapo kazini.

Majaketi hayo yatagaiwa kwa klabu za waandishi za maeneo yenye ushindani mkubwa wa kisiasa kama vile Dar es Salaam, Kigoma, Mwanza, Arusha, Mtwara, Kigoma, Zanzibar, Mbeya na Iringa.

error: Content is protected !!