August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vyanzo migogoro ya ardhi vyatajwa

Spread the love

UPUNGUFU wa vitendea kazi na watendaji katika sekta ya ardhi ndiyo sababu ya migogoro ya ardhi nchini, anaandika Regina Mkonde.

Hayo yamesemwa leo na Biseko Musiba, Mkuu wa Chuo cha Ardhi Tabora wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mchango wa vyuo vya ardhi katika wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi jijini Dar es Salaam.

“Kuna upungufu wa watendaji katika sekta ya ardhi kwa asilimia 76 na kwamba upungufu huo ndiyo sababu ya uwepo wa migogoro ya ardhi inayosababishwa na kutokupimwa kwa ardhi,” amesema.

Amesema pamoja na chuo cha Tabora kuzalisha watendaji wachache, lakini siyo wote wanaoajiriwa katika manispaa hali inayosababishwa na manispaa hizo kushindwa kuwalipa watendaji hao.

“Changamoto nyingine inayoepelekea kutokupimwa kwa ardhi ni uhaba wa vifaa, kwa sababu wanafunzi wakati mwingine hushindwa kupima ardhi kwa kukosa vitendea kazi,” amesema.

Musiba amesema kuwa, bei ghali ya vitendea kazi ndiyo changamoto inayofanya vyuo kushindwa kuwa navyo vya kutosha na kupelekea zaidi ya wananfunzi 70 kutumia darubini mbili.

Desderius Kinde, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro amesema taaluma inayotolewa na chuo chake inasaidia kupunguza migogoro ya ardhi hasa kwa wanafunzi kupima ardhi na kuweka alama.

“Wanafunzi husaidia kutatua migogoro pale wanapopima ardhi na kuweka alama kwa sababu ardhi isipowekwa alama ni rahisi kwa mtu mwenye nia mbaya kuongeza nafasi ya ardhi ya mwenzie,” amesema Kinde.

Kinde amesema lengo la vyuo vya ardhi nchini ni kutaka kuhakikisha kuwa adhma na lengo la Wizara ya Ardhi la kupima kila kipande cha ardhi pamoja na kutambulika matumizi yake inafanikiwa.

“Mwaka wa fedha ujao wa 2016/2017 Wizara imepanga kuandaa bajeti kwa ajili ya kununua vifa na kuboresha miundombinu, naamini hiyo bajeti ikitufikia changamoto zitapungua na kwamba migogoro ya ardhi itapungua kwa sababu wanafunzi watakuwa na vitendea kazi vya kutosha,” amesema.

error: Content is protected !!