Friday , 3 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Vyama vya upinzani vyavutana ushiriki chaguzi ndogo
Habari za SiasaTangulizi

Vyama vya upinzani vyavutana ushiriki chaguzi ndogo

John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema
Spread the love

 

VYAMA vya siasa vya upinzani nchini Tanzania, vimevutana katika kushiriki chaguzi ndogo za ubunge zinazotarajiwa kufanyika tarehe 9 Oktoba 2021, katika majimbo ya Ushetu mkoani Shinyanga na Konde, Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Chaguzi hizo zimeitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), baada ya aliyekuwa Mbunge wa Ushetu (CCM), Elias Kwandikwa kufariki dunia tarehe 18 Julai 2021 na aliyekuwa Mbunge mteule wa Konde (CCM), Sheha Mpemba Faki, kujiuzulu tarehe 2 Agosti mwaka huu.

Viongozi wa vyama hivyo wakizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu, leo Jumatatu, tarehe 30 Agosti 2021, baadhi yao wamesema watashiriki, wakati wengine wakisema hawatashiriki, huku wengine wakipatwa na kigugumizi.

Chaguzi hizo zimeitishwa katika kipindi ambacho baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani vikiweka msimamo wa kutoshiriki chaguzi hizo wakiishutumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutotenda haki katika michakato ya chaguzi.

Hata hivyo, NEC mara kadhaa imekanusha madai hayo ikisema kwamba inaendesha michakato ya uchaguzi kwa kufuata sheria na kanuni za uchaguzi.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera

Mkurugenzi wa Itifaki na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mrema, amesema msimamo wao wa kutoshiriki chaguzi hadi tume huru ya uchaguzi ipatikane, uko pale pale.

“Sisi tulisema hatutashiriki uchaguzi mpaka itakapopatikana tume huru, hatutashiriki uchaguzi wowote mpaka hapo tutakapokuwa na tume hiyo. Hatutashiriki na tume ambayo iliharibu uchaguzi na kuendelea kuharibu bila kuchukuliwa hatua,” amesema Mrema na kuongeza:

“Hata Konde ukiuliza kwa nini unarudiwa, tume iliharibu na kutumia gharama kubwa za wananchi kwa kurudia uchaguzi na hawajachukuliwa hatua. Tuna uhakika gani kama hawata uharibu tena?”

Kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF), kupitia Mkurugenzi wake wa Habari, Mhandisi Mohammed Ngulangwa, amesema wao hawatashiriki chaguzi hizo, kwa madai kwamba hawajaona mabadiliko yoyote.

Mhandisi Mohammed Ngulangwa, Mkurugenzi wa Habari -CUF

“Sisi bado hatujatoa msimamo tofauti na msimamo wetu wa awali, msimamo wetu kutoshiriki, kukiwa na lolote jipya tutaita mkutano na wanahabari kueleza msimamo mpya, lakini kwa sasa hatujawa na sababu za kutengua msimamo wa awali,” amesema Mhandisi Ngulangwa.

Wakati CUF na Chadema vikiendelea na msimamo wa kutoshiriki chaguzi hadi tume huru ipatikane, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na Democratic Party (DP), viko njia panda kama vitashiriki au lah.

Mwenyekiti wa Chaumma Taifa, Hashim Rungwe, amesema “hadi sasa hatujaamua kama tutashiriki, tutafanya mkutano mwishoni mwa wiki kuamua kama tunashiriki au hatushiriki.”

Katibu Mkuu wa DP, Abdul Mluya amesema “DP hatujaamua bado kama tunaenda au hatuendi.”

Chama cha ACT-Wazalendo, kupitia kwa Katibu wake wa Idara ya Uchaguzi na Kampeni, Mohammed Massaga, kimesema kitashiriki chaguzi hizo.

“Sisi tunashiriki, wagombea wamepatikana katika mchakato wa ndani. Mchakato mzima ukikamilika tutawatangazia,” amesema Massaga.

Katibu Mkuu wa Chama cha ADC Taifa, Doyo Hassan Doyo

Alipoulizwa na mtandao huu kama chama chake kitashiriki au hakitashiriki chaguzi hizo, Katibu Mkuu wa Chama cha ADC Taifa, Doyo Hassan Doyo, amesema watashiriki.

“Sisi tunashiriki, hatufanyi siasa na wenzetu tunafanya kama chama. Ndiyo maana ya vyama vingi vya siasa, askari hapambani akiwa nyumbani kuweka mazingira sawa, anapambana akiwa vitani,” amesema Doyo.

Doyo amesema, ADC imempitisha mjumbe wake wa Bodi ya Uongozi Taifa, Rehema Mjengi, kuwa mgombea Ubunge Ushetu, huku akisema Jimbo la Konde mgombea wake atapatikana hivi karibuni.

“Maana ya vyama vingi kila chama kina maamauzi yake, kama tungekuwa tunakubaliana maana yake tungekuwa na chama kimoja. Kila mmoja apambane na hali yake na sababu iliyomfanya aanzishe chama cha siasa,” amesema Doyo.

1 Comment

  • Msimamo mzuri kwa kila chama kufautana na mlivyokubaliana.

    Kila la heri katika usimamizi wa ukaguzi mdogo wa mbunge.

    Rafiki yako,

    Aliko Musa.

    Mbobezi Kwenye Majengo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Vigogo wanaokwamisha mradi Liganga na Mchuchuma kitanzani

Spread the love  NAIBU Spika wa Bunge, Mussa Zungu, watu wanaokwamisha utekelezaji...

Habari za Siasa

Gridi ya Taifa kufumuliwa kukabiliana na katizo la mgao wa umeme

Spread the love  WAZIRI wa Nishati, Januari Makamba, amesema Serikali ina mpango...

Habari MchanganyikoTangulizi

Hii hapa kauli ya Sheikh mpya mkoa wa Dar

Spread the loveSAA chache baada ya kuteuliwa kukaimu nafasi ya aliyekuwa Sheikh...

Habari MchanganyikoTangulizi

Breaking news! Mufti amng’oa Sheikh mkoa Dar

Spread the loveBARAZA la Ulamaa la Bakwata katika kikao kilichofanyika tarehe 1...

error: Content is protected !!