Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Vyama 16 vyajitosa uchaguzi mdogo Ushetu, kampeni kesho
Habari za SiasaTangulizi

Vyama 16 vyajitosa uchaguzi mdogo Ushetu, kampeni kesho

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera
Spread the love

 

VYAMA vya siasa 16, vimejitokeza kushiriki uchaguzi mdogo katika Jimbo la Ushetu mkoani Shinyanga, huku Jimbo la Konde, visiwani Zanzibar, vikijitokeza vyama vinne. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumapili, tarehe 19 Septemba 2021 na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk. Wilson Mahera, akizungumza na MwanaHALISI Online kwa njia ya simu.

Hata hivyo, Dk. Mahera amesema idadi hiyo inaweza kuongezeka kwa kuwa zoezi la uchukuaji fomu, lililoanza tarehe 13 Septemba 2021, linatarajiwa kufungwa leo majira ya saa 10 jioni.

Dk. Mahera ametaja vyama ambavyo wagombea wake wamechukua fomu za kugombea Jimbo la Ushetu, ikiwemo, Chama cha Democratic Party (DP), Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), NRA, ADC, Ada- Tadea, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo.

Vingine ni, Chama cha Demokrasia Makini, NLD na Chama Cha Kijamii (CCK), huku akisema hadi muda huo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), hakijachukua fomu.

“Katika Jimbo la Ushetu hadi kufikia tarehe 16 Septemba 2021, vyama 16 vimechukua fomu,” amesema Dk. Mahera.

Jimbo la Ushetu liliachwa wazi baada ya aliyekuwa Mbunge wake na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa, kufariki dunia tarehe 2 Agosti 2021.

Kuhusu uchaguzi wa Konde, Dk. Mahera ametaja vyama vinavyoshiriki kuwa ni, Chama cha Wananchi (CUF), CCM, AASP na ACT-Wazalendo.

“Ukienda Pemba, vimechukua vyama vinne, CUF, AASP, CCM na ACT wazalendo,” amesema Dk. Mahera.

NEC iliitisha uchaguzi mdogo katika Jimbo la Konde, baada ya mbunge wake mteule kupitia CCM, Sheha Mpemba Faki, kujiuzulu kabla ya kuapishwa kwa sababu za kifamilia.

Awali, jimbo hilo lilikuwa wazi baada ya aliyekuwa mbunge wake kupitia ACT-Wazalendo, Khatib Said Haji, kufariki dunia tarehe 20 Mei 2021.

Mkurugenzi huyo wa uchaguzi NEC, amesema mwitikio wa uchukuaji fomu katika chaguzi hizo ndogo za majimbo mawili na kata tisa, zinazotarajiwa kufanyika tarehe 9 Oktoba 2021, ni mzuri.

“Kwa ujumla mwitikio wa uchukuaji fomu ni mzuri, mpaka jioni itakapofika tutajua idadi kamili sababu bado kuna fursa za kuchukua hadi saa 10 jioni,” amesema Dk. Mahera.

Kuhusu chaguzi za udiwani, Dk. Mahera amesema wagombea wa vyama vingi wamechukua fomu za kugombea, isipokuwa katika kata za Luduga mkoani Njombe na Dongo mkoani Manyara, wamejitokeza wagombea wa CCM peke yake kuchukua fomu.

Ameongeza kuuwa kampeni za uchaguzi zinatarajiwa kuanza kesho tarehe 20 Septemba hadi 8 Oktoba mwaka huu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!