April 12, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Vyama 11 vyamjibu Zitto, vyaeleza walipo wagombea wake

zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo

Spread the love

VYAMA 11 visivyo na uwakilishi bungeni, vimeeleza mahali viliposimamisha wagombea wake, wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Maelezo hayo yamekuja siku moja baada ya vyama hivyo kuhojiwa, maeneo viliposimamisha wagombea wake, baada ya kutangaza kwamba, vitashiriki kwenye uchaguzi huo.

Akizungumza na MwanaHALISI ONLINE kwa njia ya simu leo tarehe 9 Novemba 2019, Abdul Mluya, kiongozi wa vyama hivyo,  amesema vimesimamisha wagombea katika maeneo kadhaa nchini.

Mluya amekiri kuwa, vyama hivyo havijasimamisha wagombea nchi nzima, kutokana na ukosefu wa fedha, kwa kuwa havina ruzuku.

“Sisi hata kama tungeruhusiwa kusimamisha wagombea nchi nzima tusingeweza, kwa sababu hatuna ruzuku. Tunaweka kule ambako kuna ngome zetu,” amesema Mluya.

Hata hivyo, Mluya amesema baadhi ya wagombea wake walioenguliwa wamerejeshwa. Na wengine hawajarudishwa kutokana na kukosea masharti, kwa kutosaini hati ya kiapo.

“Wajumbe wetu 2 hawajarudishwa, wamekosa sifa, hawakusaini hati ya kiapo, wakaondolewa, wengine walirudi,” amesema Mluya.

Mluya ametaja maeneo ambayo vyama hivyo vimesimamisha wagombea, ikiwemo mkoani Kigoma, ambako chama cha DP kimesimamisha wagombea kwenye vitongoji 6 na kijiji 1.

Pia, chama cha AAFP kimepita bila kupingwa katika kitongoji 1mkoani Morogoro, baada ya mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kuingia mitini.

Wakati huo huo, Mluya amesema vyama hivyo siku ya Jumanne ya tarehe 12 Novemba mwaka huu, vitafanya kikao cha kutathmini idadi ya wagombea wake, kisha vitatoa taarifa kamili ya ushiriki wao katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kwa umma.

Vyama hivyo 11 ni, Sauti ya Umma (SAU), NRA, ADC, UDP, UMD, CCK, ADA-TADEA, Demokrasia Makini, TLP na AAFP.

Miongoni mwa watu waliohoji mahali vyama hivyo viliposimamisha wagombea wao, ni Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo.

Uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba 2019, ambapo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na ACT-Wazalendo, vimesusa kushiriki uchaguzi huo.

Vyama hivyo vimesusa kwa maelezo kwamba, mchakato wa uchaguzi huo umejaa hujuma, hasa wagombea wake kuenguliwa pasina sababu za msingi.

error: Content is protected !!