January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vuta nikuvute uchaguzi wa Meya Kinondoni

Spread the love

PURUKUSHANI zimetokea kwenye uchaguzi wa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kusababisha kuahirishwa. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Miongoni mwa vyama vinavyounda Ukawa kwenye uchaguzi huo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF). Katika Manispaa ya Kinondoni Ukawa wana jumla ya madiwani pamoja na wabunge 38 huku CCM ikiwa na 27.

Zomeazomea, kelele na kejeli ziliibuka kwenye uchaguzi huo uliopangwa kufanyika kwenye ukumbi wa manispaa hiyo kabla ya zoezi la uapishaji wa madiwani na uchaguzi wa meya kufanyika.

Ukawa ndio walioanzisha kelele hizo wakitaka madiwani ambao wanatoka nje ya Dar es Salaam waondoke na kuwapisha madiwani wa Dar es Salaam pekee jambo ambalo lilizua vurugu.

Katika shughuli hiyo ya uapishaji, Ukawa walieleza kuwa baadhi ya madiwani na wabunge wa viti maalum kutoka Zanzibar ambao waliletwa ili kuwa upande wa CCM kama madiwani kutoka Jimbo la Kinondoni.

Ukawa wameeleza kuwa, sheria na taratibu za uchaguzi huo zinawanyima sifa ya kuwepo kwenye shughuli ya uchaguzu wa meya wa manispaa hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Ukawa walitaka kupata ufafanuzi kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty ili kutoa ufafanuzi juu ya hilo huku wakimtaka kuwatoa makada hao kutoka Zanzibar.

Malumbano hayo yaliyodumu kwa takribani nusu saa bila kufikia muafaka na kusababisha baadhi ya wanachama kuingia ndani ya ukumbi huo na kuleta vurugu.

Hali hiyo ilimlazimu Natty kughairisha shughuli hiyo kwa muda na kutoka nje huku akisema, atarejea baada ya saa moja ili waweze kupata muafaka.

Mkurugenzi huyo alirejea akiambatana na Mwanasheria Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Bunton Mahenge ambaye alighairisha shughuli hiyo.

“Tumeghairisha shughuli hii kutokana na kutofikia muafaka, hivyo tumeona tulipeleke suala hili mbele kwa maandishi ili kupata ufafanuzi kama madiwani hawa kutoka Zanzibari wanatakiwa kuwepo au hawatakiwi. Tumewaandikia tunasubiri majibu ya maandishi toka TAMISEMI kisha tutawajuza siku ya kuja tena.”

Akizungumza na waandishi mara baada ya kutoka nje ya ukumbi Mbunge wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika amesema kuwa ujio wa wajumbe kutoka Zanzibar ni mpango mkakati wa kikao cha Kamati kuu ya CCM kilichokaliwa juzi Ikulu ili waje kuongeza idadi ya madiwani.

“Tumezigundua mbinu zao na hawatupati. Wamezoea kuiba safari hii tupo macho, na mtindo huu wa kuwaongeza madiwani wa Zanzibar umefanyika hata katika Wilaya ya Temeke na Ilala, wanataka tuseme ili waseme tumeleta fujo kuvuruga uchaguzi sasa sisi hatutoki hadi kieleweke,” amesema Mnyika.

Pia amesema, wamebaini mbinu za CCM na nia ya kuleta madiwani hao katika kila wilaya kwa sababu CCM imepata idadi ndogo ya madiwani katika Jijin la Dar es Salaam.

Anaeleza kuwa lengo la kuongezwa kwa madiwani hao ni CCM kutaka kuongeza udadi ya kura ili wafanikiwe kutwaa nafasi ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

error: Content is protected !!