August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vodacom yadhamini ziara ya wahariri Nairobi

Spread the love

KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, ambayo ndiyo wadhamini wakuu wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara, imekabidhi hundi ya Shilingi Milioni sita kwa ajili ya kudhamini ziara ya mafunzo kwa wahariri wa habari za michezo Tanzania itakayofanyika Nairobi, Kenya kuanzia Julai 7 -11 mwaka huu, anaandika Josephat Isango.

Jacquiline Materu Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa kampuni hiyo, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari alisema wao wakiwa wadau wakubwa wa michezo nchini wameona ni fursa njema kusaidia katika ziara hiyo.

Ziara hiyo ya mafunzo imeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kwa kushirikiana na Chama Cha Waandishi wa Habari za Michezo Kenya (SJAK), ambapo wahariri 30 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini watashiriki.

“Vodacom Tanzania tunaunga mkono juhudi za TASWA katika kuwajengea uwezo wahariri wa habari za michezo na tunaamini watajifunza mengi kutoka kwa wenzao na watakuja kuyatumia mafunzo hayo katika vyombo vyao vya habari na kuwasaidia pia waandishi chipukizi wa habari za michezo,” alisema Materu.

Alisema kampuni yake imetoa Shilingi Milioni 6/- kufanikisha ziara hiyo na pia itatoa fulana maalum ambazo zitavaliwa na wahariri hao wakiwa huko.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa TASWA, Egbert Mkoko, aliishukuru Vodacom Tanzania kwa udhamini wao na kuomba kampuni nyingine zisaidie kuwaunga mkono.

“Vodacom Tanzania wameonesha ni ndugu zetu wa damu, licha ya maombi yetu ya muda mfupi kwao, lakini wametuchangia kiasi cha kutosha. Bajeti yetu bado kubwa sana kwa ziara hii, milango ipo wazi kwa wengine watusaidie,” alisema Mkoko, ambaye pia ni Mhadhiri Msaidizi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kwa mujibu wa Mkoko katika ziara hiyo, wahariri wa habari za michezo wa Tanzania watapata fursa ya kutembelea vyombo mbalimbali vya habari vya Kenya na kubadilishana mawazo na wenzao wa Kenya kuhusiana na utendaji kazi wao.

Pia alisema kutakuwa na kongamano lililoandaliwa na SJAK jijini Nairobi na litahusisha watoa mada kutoka Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS) chenye makao makuu yake Lausanne, Uswisi, ambalo pamoja na mambo mengine litajadili umuhimu wa waandishi wa habari katika kupromoti michezo.

“TASWA inaamini hii ni ziara muhimu kwa wahariri wa habari za michezo nchini na itasaidia kuboresha utendaji kazi wao,” alisema Mkoko na kuongeza kuwa pia wahariri hao watashiriki michezo na wenzao wa Kenya.

error: Content is protected !!