August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vodacom Foundation yatumia bilioni 15 katika miradi ya kijamii nchini 

Spread the love

Kampuni ya Simu ya Vodacom imetumia bilioni 15  kusaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii kupitia taasisi yake ya kusaidia masuala ya kijamii ya Vodacom Tanzania Foundation, anaandika Josephat Isango.

Katika kipindi cha miaka 10 taasisi ya Vodacom Tanzania imekuwa ikifanya kazi na taasisi za serikali na wadau wengine kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi wengi hususani katika sekta za elimu , afya na uwezeshaji wa kuinua makundi mbalimbali kiuchumi.

Taarifa iliyotolewa inamnukuu Rosalynn Mworia Afisa Mtendaji wa  Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom Tanzania, akisema kuwa matumizi ya teknolojia yameboresha mabadiliko ya wananchi kuwa bora.

“Tumeshirikiana na serikali na wadau wengine kuboresha huduma za elimu,afya na kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi”.Baadhi ya miradi ambayo imeleta mabadiliko makubwa kwa jamii ni mradi wa kuwawezesha wasichana wa Hakuna Wasichoweza na mradi wa kuelimisha masuala ya afya na uzazi ujulikanao kama Wazazi Nipendeni.”. alisisitiza

Kwa mujibu wa ripoti ya Vodacom Tanzania Foundation imebainishwa kuwa kuanzia mwaka 2006 hadi imetumia shilingi bilioni 15 kwa kufadhili miradi ipatayo 130 ya kijamii lengo kubwa likiwa ni kuleta mabadiliko kwa kuboresha maisha ya wananchi kwenye jamii.

Uboreshaji wa maisha ya wananchi umefanika kwa kutumia teknolojia ya mtandao wake kuboresha huduma mbalimbali na kuokoa maisha ya wananchi kupitia miradi mbalimbali.

Vodacom Tanzania Foundation imekuwa ikitumia teknolojia katika miradi ya kuboresha huduma za uzazi na kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga kupitia huduma ya kutuma na kupokea pesa ya ijulikanao kama M-Pesa.

Moja ya mradi huu wa kuokoa maisha ya akina mama wajawazito kupitia huduma ya M-Pesa unaendeshwa katika wilaya za Sengerema na mkoani Shinyanga ambao unafanika kwa kushirikiana na  madereva wa teksi.Madereva waliosajiliwa katika mradi huweza kuwawahisha akina mama wajawazito katika vituo vya afya waonapo dalili za kujifungua ambapo madereva hao hupatiwa malipo yao kupitia simu zao za mkononi na umeonesha mafanikio makubwa ukiwa umeweza kuokoa maisha ya akina mama wajawazito na watoto wachanga wapatao 225 kwa mwezi.

Mradi mwingine ambao Vodacom Tanzania Foundation imeufankisha na umeleta mabadiliko makubwa ni mradi wa kutokomeza ugonjwa wa Fistula ambao imeuendesha kwa kushirikiana na taasisi ya Comprehensive Community Based Rehabilitation in Tanzania (CCBRT).

Kupitia huduma ya M-Pesa akina mama waliobainika kuwa na ugonjwa wa Fistula walikuwa wakilipiwa gharama za usafiri za kuwawezesha kufika katika hospitali ya CCRBT kupatiwa matibabu bila malipo na wakipona wanaripiwa gharama za kurejea makwao.Mradi huu umeweza kuwanufaisha akina mama wapatao 2, 482.

Kwa upande wa elimu ,Vodacom Tanzania Foundation imewezesha wanafunzi kutoka shule za msingi na sekondari kuingia katika ulimwengu wa kompyuta kwa kusaidia kuzipatia vifaa vya maabara za kompyuta ili waweze kusoma somo hilo kwa nasharia na vitendo.Kwa kushirikiana na kampuni ya Samsung imekuwa ikiendesha mradi wa Smart School ambao umekuwa na mafanikio makubwa na kuwanufaisha wanafunzi zaidi ya 8,000 kwa kupatiwa laptop ,vifaa vya kujifunzia kwa njia ya mtandao wa kidigitali na kuunganisha mtandao wa interneti mashuleni.

Katika mradi wa Hakuna Wasichoweza ambao unatekelezwa kwa ushirikiano na shirika lisilo la kiserikali la T-MARC katika mikoa ya Lindi na Mtwara umefanikiwa kupunguza utoro kwa wasichana mashuleni  uliokuwa unatokana na changamoto za vipindi vya hedhi kwa kutokuwa na vifaa vya kuwakinga na shule zao kutokuwa na miundombinu ya kuwawezesha kujiweka vizuri katika kubaliana na hali hiyo.

Kupitia mradi huu wasichana wanapatiwa elimu ya afya ya uzazi na kuwapatia taulo za kujihifadhi wanapokuwa kwenye vipindi vya hedhi na hadi sasa zaidi ya wasichana 5,000 wamenufaika na mradi huu.

Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation pia imekuwa ikishirikiana na serikali kupitia Wizara ya Afya katika miradi ya kufikisha jumbe za kuelimisha masuala ya afya bure kwa wananchi kupitia mtandao wa Vodacom  na zaidi ya wananchi milioni 1 wanaendelea kunufaika na huduma hii.

Kwa kutumia bilioni 15 ndani ya kipindi cha miaka 10, taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation imeboresha maisha ya watanzania wengi na inaendelea kutimiza dhamira yake ya kuunga mkono jitihada za serikali za kupambana na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii na kubadilisha maisha ya watanzania kutoka hali duni kuwa bora

 

error: Content is protected !!