July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vodacom Foundation kusafirisha wagonjwa wa Saratani

Spread the love

TAASISI ya Vodacom Foundation imetoa ufadhiri wa kugharamia usafiri kwa wanawake wenye saratani ya mlango wa kizazi kufika katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) za Dar es Salaam na Bugando, Mwanza ili kupata matibabu. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea).

Msaada huo wa Vodacom Foundation, unalenga kupunguza idadi ya vifo vya wanawake vinavyokadiliwa kuwa zaidi ya 4,000 kwa mwaka vinavyotokana na kansa ya mlango wa kizazi, ukosefu wa huduma kwa hatua za awali za ugonjwa huo.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Beatrice Erasto ametoa shukrani za pekee kwa Vodacom Foundation kwa kujitolea kusafirisha wanawake wanaogundulika na ugonjwa huo kutoka mikoa ya Iringa, Mbeya na Mwanza.

Beatrice amesema kupitia mradi huo tayari wanawake 17 wameshafikishwa katika hospitali ya ORCI ya Dar es Salaam, kati yao watatu washaruhusiwa, saba wanaendelea na matibabu huku sita wakisubiri matibabu.

Aidha amewataka wanawake kujitokeza kujua dalili za awali za ugonjwa huo, na wale watakaogundulika na dalili za awali watapata huduma bure.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa asasi isiyo ya kiserikali inayojikita Katika Kuboresha Afya Tanzania, T-MARC Tanzania, Diana Kisaka amesema Tanzania ni mojawapo ya nchi zenye mzigo mkubwa wa saratani ya mlango wa kizazi duniani, hali inayopelekea wanawake zaidi ya 4,000 kufariki kila mwaka, sawa na wanawake 11 kila siku.

Amesema anategemea wakina mama kujitokeza mara kwa mara kupima afya zao kwani ikigundulika mapema saratani ya mlango wa kizazi inatibika.

Hata hivyo amechukua nafasi hiyo kuwashukuru Vodacom Foundation, pamoja na washiriki wengine kwa msaada wa hali, mali na utaalamu katika kutibu saratani ya shingo ya kizazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Vodacom Foundation, Renatus Rwehikiza amesema taasisi yake inadhamira ya kuendelea kusaidia na kuhakikisha Watanzania wanapata misaada itakayopelekea kupata uuduma stahiki.

Rwehikiza amesema msaada huo utapunguza vifo vya wanawake vinavyotokea mara kwa mara kutokana na ukosefu wa huduma za haraka za usafiri kufika katika vituo husika, hivyo itasaidia kupunguza asilimia ya vifo.

Mashirika mengine yaliyojitokeza ni Pink Ribbon Red Ribbon (PRRR), Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA), Tanzania Youth Association (TAYOA), Wanawake na Maendeleo (WAMA) na Mbeya HIV/AIDS Network (MNHT).

error: Content is protected !!