June 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Vituo vya afya vyatakiwa kuwa na wataalam wa kutosha

Spread the love

HALMASHAURI zote nchini zimetakiwa kuwa na vituo vya afya vilivyo na wataalamu waliosomea, dawa na vifaa tiba vya kutosha ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, anaandika Happyness Lidwino.

Imeelezwa kuwa, endapo wajawazito watajifungulia katika vituo vya afya vyenye huduma zote, watafanikiwa kuondokana na changamoto hiyo.

Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Utepe Mweupe wa Uzazi Salama, Samia Suluhu, Makamu wa Rais amesema kuwa, katika kulitafutia ufumbuzi suala la kuepusha vifo vya akinamama wanaojifungua,   halmashauri zijikite katika kuongeza vituo vya afya.

Lakini pia kuhakikisha wanapata watoa huduma wenye ujuzi na stadi za kuokoa maisha, ikiwa ni pamoja na upasuaji wa kutoa mtoto na upatikanaji wa damu salama.

“Tumeungana leo kwa pamoja na wadau mbalimbali kwa lengo la kuwakumbuka wanawake wote waliopoteza maisha kwasababu mbalimbali za uzazi lakini pia kuangalia mikakati madhubuti itakayofaa katika kuondokana na hali hiyo kuendelea nchini,.

“Kwa kulizingatia hilo, serikali kwa kushirikiana na wadau wote tuongeze kasi katika mpango mkakati wa kupunguza vifo vya wanawake wajawazito, watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano.

“Mpango huo ni angalau asilimia 50 ya vituo vyote hapa nchini viwe vinatoa huduma ya upasuaji na damu salama;hivyo basi linawezekana kila mkoa endapo kila halmashauri italizingatia hili,”  amesema Suluhu.

Akizungumzia kwa upande wa Hospitali za Wilaya, makamu huyo amesema ni lazima ziwe na huduma kamili za uzazi salama kwa asilimia mia moja.

“Ninatarajia kuona hospitali za wilaya zinatoa huduma zote na ninatarajia kuliona mara tu mipango ama bajeti za halmashauri zote kwa mwaka wa fedha 2016/2017 zitakapopatikana.

“Lakini pia nina uhakika  halmahauri zikiwajibika na kufanya  tathimini ya umbali wa ulioko kati kituo chenye huduma za upasuaji na damu salama na waliko wananchi basi vifo vitapungua sana,” amesema.

Akizungumzia kuhusu tafiti zilizofanyika hapa nchini kwa takriban miaka 20 iliyopita, amesema idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi vimekuwa vikipungua lakini kwa kasi ndogo.

Amesema, kwa mwaka 1996 kulikuwa na vifo 529 kwa kila vizazi hai 100,000 na kufikia vifo 432 kwa kila vizazi hai 1000,000 mwaka 2012 huku ripoti ya Umoja wa Mataifa ikionyesha vifo 410 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2014.

Aidha amesema, takwimu hizo ni sawa na vifo 7,500 kwa mwaka vitokanavyo na uzazi na kuongeza kuwa kwa upande wa vifo vya watoto wachanga walio chini ya mwezi mmoja hupatikana vifo 21 kwa kila vizazi hai 100,000.

Mratibu wa Muungano wa Utepe Mweupe wa Uzazi Salama Tanzania, Rose Mlay, ametoa rai kwa serikali ya awamu ya tano kuhakikisha inatenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuhudimia akinamama wajawazito.

 

error: Content is protected !!