August 12, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vituo maalum vya kuuza mkaa kuanzishwa

Spread the love

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)  wanakusudia kuanzisha vituo maalumu kwa ajili ya uuzaji mkaa ili kupambana na uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti na kuchoma mkaa, anaandika Dany Tibason.

Hayo yalielezwa na Prof. Dos Santos Silayo Mtendaji Mkuu wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)  alipokuwa akizungumza na  Mwanahalisi online ambapo alikiri uwepo wa changamoto ya uuzaji wa mkaa kiholela.

Profesa Silayo amesema uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa ni mkubwa sana na bila udhibiti unaweza kusababisha kuwepo kwa jangwa hapa nchini.

“Vibali vya ukataji mkaa vinatakiwa kutolewa kwa umakini na viongozi ili kuepuka kuendelea kwa uharibifu wa mazingira sisi TFS tunatoa elimu ya utunzaji wa mazingira na utengenezaji wa majiko yanayoweza kutumia nishati mbadala kwa kupunguza kasi ya matumizi ya mkaa,” amesema.

Mathew Kiondo Meneja wa TFS kanda ya kati amesema, kila mwaka wakala wa misitu hupeleka sampuli ya asali  nchini Ujerumani kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hivyo uvumi kuwa asali inayozalishwa nchini hususani inayotoka Mkoa wa Tabora ina madini ya Nicotine si sahihi.

“Napenda kuwatoa wasiwasi watanzania na wale ambao wapo nje ya Tanzania kuwa asali ya inayovunwa hapa nchini ni salama na ina viwango vinavyokubalika katika soko la dunia,” ameeleza Kiondo.

error: Content is protected !!