April 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Vituko vitupu uchaguzi serikali za mitaa

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Spread the love

KATIKA mitaa 565 jijini Dar es Salaam, kwa mujibu wa tovuti ya mkoa huo, mitaa isiyozidi mitano, iliyoripotiwa kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, jana tarehe 24 Novemba 2019. Anaripoti Waandishi Wetu … (endelea).

Mitaa iliyoripotiwa kufanya uchaguzi huo, ni Mtaa wa Darajani, Kimanga, kata ya Tabata na Malapa, kata ya Buguruni. Yote hiyo, ipo katika halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

Kwa upande wa Manispaa ya Kinondoni, uchaguzi umefanyika katika mtaa wa Mikoroshini, kata ya Msasani; huku kwenye manispaa ya Temeke, waandishi wa habari walishuhudia kutokuwapo kufungwa ofisi za wasiamizi wa uchaguzi na kutokuwapo vifaa vya uchaguzi katika maeneo kadhaa, ikiwamo kata ya Mbagara Kibonde Maji.

Mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Azam TV, amenukuliwa akiripoti kuwaona wananchi, wakisota kwenye vituo vya kupigia kura, kufutia kufungwa kwa ofisi hizo za wasimamizi.

Anasema, wananchi hao ni miongoni mwa waliojitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi huo, uliotangazwa kufanyika jana nchini kote.

Uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kwa mwaka huu wa 2019, umevurugika karibu nchini kote, kutokana na kususiwa na vyama vya upinzani kwa maelezo kuwa umechakachuliwa.

Kata ya Wazo iliyo na mitaa mine, ilifungwa muda wote huku wananchi wachache wakijitokeza kupiga kura bila mafanikio yoyote.

Wananchi hao, waliueleza mtandao huu kwamba wamejitokeza kupiga kura lakini wamekuta vituo vimefungwa na hakuna maelezo wala mtu wa kuulizwa.

“Sina namna, sijui kwanini hawajafungua. Sio mimi tu, wengine wameondoka bila kuwa na taarifa yoyote,” amesema mpiga kura aliyejitambulisha kwa jina la Lazaro Msuya.

Hali ya Wazo inafanaa na ile ya Kijitonyama, ambapo hakuna ofisi ambayo ilifunguliwa kwa ajili ya upigaji kura.

Kituo cha kupigia kura cha shule ya Msingi Mwananyamala Mchangani, Kinondoni mpaka kufika saa nne asubuhi, kilikuwa hakijafunguliwa, wala vifaa vya uchaguzi havikuwepo.

Wananchi wachache waliojitokeza, walisubiri huku wengine wakirejea makwao kutokana na kukosa taarifa zozote zinazohuu uchaguzi.

Kwenye maeneo uchaguzi ulipofanyika jijini humo, vyama vilivyoingiza wagombea ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Alliance Democratic for Change (ADC).

Mgombea wa nafasi ya ujumbe kwenye kata ya Malapa kupitia ADC, Ramadhani Ngubi aliiambia MwanaHALISI kutoridhishwa na uratibu wa uchaguzi huo akidai, “wasimamizi wa uchaguzi wamevunja makubaliano yao.”

“Tangu mwenendo wa kuchukua na kurejesha  fomu na mpaka sasa sio mzuri, mimi nikiwa kama Katibu wa ADC…” ameeleza Ngubi.

Hata hivyo, Is’haka Nyota (CCM) ambaye ni mwenyekiti aliyepita bila kupingwa amesema, uchaguzi umekwenda vizuri, ingawa kulikuwa na mvua.

“Uchaguzi uko vizuri na hakuna lolote baya.., mtu anayesema vituo vimehamishwa, tulishatangaziwa watu watapiga kura pale walipojiandikisha,” amesema Nyota.

Katika baadhi ya mikoa, nembo za vyama vilivyojitoa Chadema, CUF, ACT-Wazalendo na vingine – zimeonekana kwenye karatasi za kupigia kura.

Kwenye manispaa ya Shinyanga, katika mitaa minne – Ibadakuli, Mwamalili, Kambarage na Ndembezi – nembo za CUF, Chadema na ACT-Wazalendo, zilionekana kwenye karatasi ya kura.

Rajabu Masanche, msimamizi wa uchaguzi kwenye manispaa hiyo amesema, wagombea hao hawakuwasilisha barua za kujitoa, licha ya kutakiwa kufanya hivyo na viongozi wao wakuu.

Nembo hizo zimejitokeza kwenye maeneo mengine ikiwemo Singida katika Halimashauri ya Ikungi. Nembo zilizoonekana kwenye uchaguzi huo licha ya vyama kugomea ni CUF, Chadema na ACT- Wazalendo.

Justice Kijazi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo amesema, watu wamejitokeza na kura zilipigwa.

John Mrema, Mkurugenzi wa Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje amesema, chama hicho kitatafakati hatua za kuchukua baada ya serikali kulazimisha kuweka nembo ya chama chao.

Abdul Kambaya, Mkurugenzi wa Mawasiliano CUF amesema, chama hicho kilijiondoa kwenye uchaguzi huo na kwamba hawafuatilii chochote kinachohusu uchaguzi huo.

error: Content is protected !!