Sunday , 2 April 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Viti Maalum Chadema pasua kichwa, CC yaahirishwa
Habari za SiasaTangulizi

Viti Maalum Chadema pasua kichwa, CC yaahirishwa

Tundu Lissu, Mgombea Urais Tanzania (Chadema).
Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Mendeleo (Chadema) nchini Tanzania, kiko njiapanda juu ya kuamua kupendekeza majina ya wabunge wa viti maalum kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Chadema na Chama tawala-Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndivyo vyenye sifa ya kupendekeza majina ya wabunge wa viti kwa NEC ili iweze kuwateua kuwa wabunge.

Hatua hiyo ni baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano ya tarehe 28 Oktoba 2020 na CCM kujikusanyia madiwani na wabunge wengi pamoja na nafasi ya Urais.

Chadema imekuwa katika mjadala mzito ndani na nje ya chama hicho wa je, wapendekeze majina ya wabunge wa viti maalum au isifanye hivyo, hasa ikizingatiwa, imekwisha ueleza umma wa Watanzania kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi huo.

Tarehe 31 Oktoba 2020, viongozi wakuu wa Chadema na ACT-Wazalendo, walizungumza na waandishi wa habari na kutaka uitishwe upya uchaguzi mkuu wa Zanzibar na Tanzania kwa kutumia Tume Huru ya Uchaguzi.

Viongozi hao wakiongozwa na wenyeviti, Freeman Mbowe wa Chadema na Maalim Seif Sharif Hamad wa ACT-Wazalendo, walidai uchaguzi huo uligubikwa na ukiukwaji wa sheria, kanuni na miongozo.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Kutokana na misimamo hiyo, kumekuwa na mijadala ndani na nje ya Chadema juu ya chama hicho kupeleka majina NEC ya viti maalum ambapo wapo wanaodai yapelekwe na wengine wanasema “kupeleka majina hayo ni kuhalalisha kuwa uchaguzi ulikuwa hauna tatizo.”

Pia, wanadai, kupeleka majina hayo yatakiwezesha chama kupata ruzuku itakayosaidia kuendesha chama huku kikiwa kinajipanga zaidi kwa chaguzi zijazo.

Wapo wanaodai, Chadema ikipeleka wabunge wa viti maalum bungeni, itawawezesha kupata sehemu ya kuzungumzia ndani ya Bunge, ingawa wapo wanaosema “kwenda bungeni, haitakuwa na maana na Chadema itakuwa inajichimbia shimo yenyewe.”

Mbunge mteule wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Khenani akijisajili katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo Jumapili

Ugumu wa hoja hizo zote, zimeifanya Kamati Kuu ya Chadema (CC), iliyokuwa imekutana jana Jumamosi tarehe 7 Novemba 2020 jijini Dar es Salaam, kujadili masuala mbalimbali ikiwemo hilo ambalo hawakufikia mwafaka na kuamua kuahirisha kikao hadi wakati mwingine.

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, zinadai ni wajumbe wasiozidi saba akiwemo Mbowe, hawataki kupeleka majina NEC kwani wanasema “itakuwa kuwahadaa wananchi, ambao wamewaeleza hawakubaliani na matokeo.”

Mmoja wa wajumbe wa kamati kuu amesema “tumeshindwa kukubaliana bado. Wanaopinga wasiende ni wachache kuliko wanataka waende. Kutokana na hilo, mwenyekiti (Mbowe) aliona ni burasa kuahirisha kikao.”

Amesema, kwa sababu tamko la kutotambua matokeo hayo yalitolewa na vyama viwili- Chadema na ACT-Wazalendo, watajadiliana nao kwanza kabla ya kutoka na uamuzi wa mwisho wa ama kushiriki au la.

Halima Mdee, Mgombea Ubunge wa Kawe kwa tiketi ya Chadema

Katika moja ya andiko la aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chadema, Tundu Lissu yeye anapingana na kupeleka wabunge wa viti maalum bungeni.

“Nadhani kuna haja ya kutenganisha ‘maslahi ya chama’ na maslahi binafsi ya baadhi ya wanachama wake katika jambo hili. Kila mmoja anadai msimamo wake ni kwa ‘maslahi ya chama.”

Tayari, Katibu wa Bunge la Tanzania, Stephen Kagaigai akizungumza na waandishi wa habari jana Jumamosi alisema kikao cha kwanza cha Bunge Jipya la 12 kitaanza Jumanne tarehe 10 Novemba 2020.

Kagaigai alisema, usajili wa wabunge na taratibu za kibunge, zimeanza jana Jumamosi.

Kwa upande wake, Tundu Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bada) anasema “Ninahisi kuwa kuna baadhi ya watoa hoja, kwa sababu ya nafasi zao, wana fursa ya kufaidika binafsi na uamuzi wa kushiriki bungeni au kwenye halmashauri. Kutokushiriki kutawaathiri wanachama hao moja kwa moja.”

“Hata hivyo, badala ya kukiri kwamba kushiriki kutawapatia faida binafsi na kutokushiriki kutaondoa ‘fursa’ hizo, watu hao wanajificha kwenye kichaka cha ‘maslahi ya chama’!!!”

Lissu anaendelea kusema “Je, chama kina maslahi gani kwenye kuhalalisha uchafuzi wa tarehe 28 Oktoba kwa kukubali kushiriki makombo yanayotokana na karamu ya wachafuzi???. Kama suala ni kukosa ruzuku, tuzungumzie namna ya kutafuta pesa ya ku-replace loss ya hiyo ya ruzuku bila kuhalalisha ubakaji uliofanyika tarehe 28 Oktoba.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia apangua mawaziri

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la...

Habari za Siasa

RC mstaafu afariki dunia, CCM yamlilia

Spread the loveALIYEWAHI kuwa mkuu wa mikoa ya Dodoma, Mara, Mtwara na...

Habari za Siasa

Marekani kuwekeza Dola 500 Mil kupeleka bidhaa na huduma Tanzania

Spread the loveMAKAMU wa Rais wa Marekani, Kamala Harris amesema miongoni mwa...

Habari za Siasa

Kamala ataja hatua mpya kuimarisha uhusiano wa kibiashara Tanzania, Marekani

Spread the loveKATIKA kuimaridha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya Tanzania...

error: Content is protected !!