Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Viti Maalum Chadema: NEC yabebeshwa mzigo
Habari za Siasa

Viti Maalum Chadema: NEC yabebeshwa mzigo

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera
Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania, kueleza Watanzania ilipopata majina 19 ya wanachama walioteuliwa kuwa wabunge wa Viti Maalum kupitia chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano tarehe 25 Novemba 2020, jijini Dar es Salaam, John Mnyika ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho amesema, mwenye mamlaka ya kuteua majina hayo kwa mujibu wa Katiba ya Chadema ni Kamati Kuu ambayo mpaka sasa hajateua.

Jana Jumanne tarehe 24 Novemba 2020, Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwaapisha wanachama 19 wa Chadema kuwa wabunge wa Viti Maalum kupitia chama hicho.

Baada ya kuwaapisha viwanja vya Bunge, Spika Ndugai alisema, alipokea barua ya uteuzi wa majina hayo kutoka NEC tarehe 20 Novemba 2020.

          Soma zaidi:-

Wanachama hao walioongozwa kuapishwa na Halima Mdee, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema  (Bawacha), walidai uteuzi wa majina yao ulipata baraka zote za chama hicho.

“Chadema hakijateua wabunge wa viti maalumu au wagombea ubunge viti maalumu, wala hakijawasilisha orodha yoyote ya uteuzi wa wabunge viti malaumu, NEC ieleze majina hayo imepata wapi,” amesema Mnyika na kuongeza:

“Kwa Katiba ya Chadema, mamlaka ya uteuzi wa wabunge yako kwa Kamati Kuu ya chama Ibara ya 7.7 ambayo inasema, moja ya kazi ya Kamati Kuu ya chama ni kuthibitisha uteuzi wa wagombea. Kamati Kuu ya chama haijawahi kufanya kikoa cha kuteua majina ya wabunge wa Viti Maalunu,” amesema Mnyika.

Mnyika amesema, Katiba ya Chadema inaelekeza Katibu Mkuu kuwasilisha orodha ya majina hayo NEC, jambo ambalo yeye hajalifanya.

“Pili, Katibu Mkuu wa chama mwenye mamlaka ya kimawasiliano ya kuwasiliana na NEC, sijawahi kuwasilisha orodha yoyote NEC ya wanaoitwa waliopendekezwa kuwa wabunge viti maalumu,” amesema Mnyika.

Mnyika amesema, Chadema kimeshangazwa na uteuzi huo kwa kuwa, iliwasilisha taarifa rasmi NEC kwamba, haijateua wabunge hao na kwamba, tume hiyo kupitia barua ya tarehe 10 Novemba 2020 iliijibu Chadema, ikikiri kutopokea orodha hiyo.

Mwenyekiti wa NEC, Semistocles Kaijage

Amesema, NEC kupitia kwa mkurugenzi wake, Dk. Wilson Mahera, ilikiri kwamba chama hicho hakijawasilisha majina hayo na kukitaka Chadema kufanya hivyo huku akipewa na fomu namba 8(d) ambazo zinapaswa kujazwa na wanaopendekezwa.

“Mawasiliano yangu ya mwisho NEC zilikuwa barua mbili,  barua ya kwanza tumekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara kwenye masuala mbalimbali ya uchaguzi, barua ya mwisho niliiandika  tarehe 9 Novemba 2020 kwenda kwa  mkurugenzi NEC.”

“Barua hii niliiandika baada ya mkurugenzi huyo kunukuliwa kwenye vyombo vya habari akisema, Chadema imewasilisha orodha ya viti maalumu, kwamba NEC imewasilisha bungeni majina 19 ya wabunge kupitia Chadema,” amesema Mnyika na kuongeza:

“Baada ya barua hiyo, NEC wakajibu barua hiyo kwenda Katibu Mkuu Chadema, katika barua hiyo iliyosainiwa na Dk. Mahera (Wilson Mahera, Mkurugenzi wa Uchaguzi) tareh 10 Novemba ikakiri Chadema haijawasilisha orodha yoyote.”

“Tume ikaandika barua kutoa mwito kwa Chadema kuwasilisha orodha na sio orodha peke yake pamoja na fomu namba 8(d) ambayo kipengele C inapaswa kusainiwa na katibu mkuu,” amesema Mnyika huku akionyesha fomu hizo 113 alizozipokea kutoka NEC

“Kwa hatua hiyo, NEC ijitokeze hadharani, ieleze hiyo orodha iliwasilishwa na nani, nani aliyesaini eneo la katibu mkuu ikiwa mimi sikufanya hivvyo au naibu wangu,” amesema Mnyika

Baada ya mkutano huo na waandishi kumalizika, MwanaHALISI Online lilimtafuta Dk. Mahera ili kupata ufafanuzi juu ya madai ya Mnyika, hata hivyo hakupokea simu.

Halima Mdee, Mbunge wa Chadema Viti Maalim

Badala yake, Dk. Mahera alituma ujumbe mfupi wa maneno uliosema “samahani, siwezi  kuzungumza kwa sasa.”

Hata alipoulizwa kwa kutumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kwamba NEC ilipata wapi orodha ya majina ya wanachama wa Chadema iliyowateua kuwa wabunge Viti maalumu, hakujibu mpaka habari hii inaandikaa.

Kilichotokea kwa Dk. Mahera ndivyo imekuwa kwa Mwenyekiti wa NEC, Semistocles Kaijage alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita pasina kupokelewa.

Jitihada za kuwatafuta wawili hao zinaendelea.

2 Comments

  • Uchoyo wa wakubwa wangeshinda yote haya yasitokee wana wivu akina mama hao kupata ulaji. Hawana nia njema na nchi yao.

  • Hapa ndipo CCM walipotufikisha! Wamevuruga mifumo yote ya sheria, haki na utawala bora! Wamevuruga Bunge, Polisi, Mifumo wa sheria, Usalama na Ulinzi! Sasa ni vigumu kutarajia hukumu ya haki Mahakamani, kutarajia haki toka polisi, au vyombo vya dola ambavyo kimsingi ni vya wananchi! Tume inavunja Katiba, Polisi wanavunja Katiba, Mahakama inapata vigugumizi katika maamuzi, Watendaji wa serikali wanavunja Katiba bila ya kukemewa wala kuchukuliwa hatua! Hakuna pa kushtaki! Mahakama ya Afrika Mashariki Mashariki serikali imejitoa, Mahakama ya Afrika serikali imejitoa. Serikali imekazana kutunga sheria za kulinda wahalifu dhidi ya umma! Sijui kinga za kushtakiwa Spika na Naibu wake zina manufaa gani! Katika maigizo ya uchaguzi uliopita TUME iliyoundwa na serikali ya walewale walioshika dola imeliaibisha Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!