January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vitambulisho vya kupigia kura, mradi feki

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva

Spread the love

MRADI wa vitambulisho vipya vya kupigia kura nchini, umeshindwa kabla ya kuanza. Vitambulisho vipya vya taifa vitaandaliwa kupitia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR).

Mfumo huu unatumika kuchukua au kupima taarifa za mtu za kibaiolojia au tabia za mwanadamu na kuzihifadhi katika kazidata (database) kwa ajili ya utambuzi.

Gharama za mradi huu unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh. 293 bilioni. Umepangwa kuanza Septemba 2014.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, ameeleza wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, mpango huo ni “sehemu ya mchakato wa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura.”

Kushindwa kwa mradi huu, kumesababishwa na yafuatayo:

Kwanza, mfumo huu unahitaji kuwapo kwa vifaa vya kisasa – komputa, kamera, kifaa cha kuchukulia alama za vidole na mashine ya kutotoa vitambulisho (printa).

Vifaa hivi vinavyohitajika, vinatumia umeme, tena wa uhakika. Katika maeneo mengi ya nchi hayana umeme. Machache yaliyobahatika kuwa na umeme, yamekuwa yakikumbwa na mgawo wa mara kwa mara.

Mpaka sasa, serikali kupitia Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO), wameshindwa kufikisha umeme nchi mzima. Taarifa za serikali zinaonyesha, ni asilimia 30 ya watu wote ndiyo waliobahatika kupata umeme.

Nchini Bolovia, mashine hizi zilitumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2009. Lakini kabla ya kuziingiza katika uchaguzi, taifa hilo lilitoa mafunzo kwa maelfu ya maofisa wa usimamizi wa uchaguzi kwa miezi kadhaa.

Hata hivyo, siku ya uchaguzi ilipowadia, mitambo yao ilikwama kufanya kazi. Zilitolewa sababu mbili: Virusi kuingilia mfumo wa utendaji wa komputa na kufuta baadhi ya taarifa na kutokuwapo mtandao wa uhakika wa intaneti, hasa vijijini. Matatizo kama hayo yanaweza kutokea nchini.

Pili,tekronojia hii ya BVR ni mpya. Lakini mpaka sasa, haijafanyia majaribio nchini. Mitambo hii inahitaji wataalam wa kutosha – kutoka ndani na pengine nje ya nchi.

Haifahamiki kama NEC imetenga fedha za kutosha kwa kazi hiyo. Kinachojulikana, ni malalamiko kuwa serikali imeidhinisha kiasi kiduchu katika mradi huu. Bunge la bajeti limeidhinisha kiasi cha Sh. 7 bilioni, wakati mradi unagharimu kiasi cha Sh. 293 bilioni.

Aidha, kila uchaguzi nchini, NEC hutumia watendaji wa kata, vijiji na halmashauri za wilaya na walimu wa shule za msingi katika kazi ya kuandikisha, kusimamia na kuendesha. Idadi kubwa ya wanaotumwa na NEC katika chaguzi hizo, hawafahamu hata kutumia kompyuta.

Tatu,serikali inakiri kuwapo kwa tatizo la umeme nchini. Lakini inasema, itatumia umeme unaozalishwa kwa njia ya jua. Umeme huu utafungwa kwenye magari maalum.

Hata hivyo, NEC inajua kwamba taifa hili halina miundombinu mizuri ya barabara. Maeneo mengine, hata baiskeli hazifiki. Hivyo basi, kukosekana kwa barabara bora, kutasababisha magari hayo “maalum” kushindwa kufika katika baadhi ya maeneo.

Nne, NEC wanasema, itatumia mtambo wa BVR kuandikisha wapigakura na siyo kupigia kura. Ni utaratibu uleule wa miaka nenda rudi. Lakini wanasema, hawatatumia vidole kumtambua mpigakura.

Sasa swali la kujiuliza: Ikiwa kazi ya BVR ni kuandikisha wapigakura, mfumo huu una faida gani katika kuzuia udanganyifu wakati wa kupiga kura? Mfumo huu utakuwa na faida gani katika kuzuia wapigakura hewa au kuhesabu kura? Utatoa tiba ipi kwa wanaoandikishwa mara mbili?

Wanaoandaa mfumo mpya wa BVR na ambao utameza mamilioni ya shilingi za walipa kodi, hawaoni kuwa tatizo la utambuzi wa mpigakura litabaki pale pale?

Tungeelewa kama mfumo wa BVR ungetumika katika kuandikisha, kuhifadhi na kupiga kura. Ungetumika katika kuzuia watu kujiandikisha mara mbili; na au kuzuia vituo hewa vya kupigia kura.

Lakini kwa hili la sasa, ambako hata yule asiyekuwa na kitambulisho bado aweza kupiga kura, huu ni mradi usiokuwa na tija. Hauhitajiki.

Mashine za mradi huu zimenunuliwa kwa fedha nyingi. Taarifa zinasema, gharama za mashine hizi zimepandishwa zaidi ya mara 10 na genge la wajanja wachache serikalini.

error: Content is protected !!