May 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

‘Vita nyingine’ ya uchaguzi mdogo yaja

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage

Spread the love

KIPYENGA cha uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo matatu ya Tanzania Bara na kata sita, kimepulizwa rasmi, imefahamika, anaandika Faki Sosi.

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud Hamid, ametaja majimbo kutakakofanyika uchaguzi kuwa ni Singida Kaskazini, Longido na Songea Mjini.

Uchaguzi katika jimbo la Singida Kaskazini unafanyika kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Lazaro Nyalandu.

Nako katika jimbo la Longido, uchaguzi wa mbunge unafanyika kufuatia Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, kumvua ubunge mbunge wake, Onesmo Nangole.

Mbunge huyo wa Chadema amekuwa mbunge wa kwanza kupoteza jimbo lake baada ya mahakama kutengua matokeo ya ushindi wake yaliyotokana na uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015 na kuamuru kurudiwa upya.

Ushindi wa Nangole aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Arusha na ambaye alikihama chama hicho na kujiunga na upinzani, ulipigwa mahakamani na aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM, Stephen Kiruswa.

Katika jimbo la Songea Mjini, uchaguzi mdogo unafanyika kufuatia kifo cha mbunge wake, Leonidas Gama.

Naye waziri wa serikali za mitaa kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, ameitaarifu NEC kuwepo nafasi wazi za madiwani katika kata sita Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa Jaji Hamid, uteuzi kwa wagombea katika majimbo ya Singida Kaskazini na Longido na kata hizo sita, utafanyika tarehe 18 Desemba 2017, na uteuzi wa wagombea katika jimbo la Songea Mjini utafanyika 20 Desemba 2017.

Uchaguzi huo mdogo wa ubunge na udiwani umepangwa kufanyika tarehe 13 Januari 2018.

Amezitaja kata ambazo zitafanya uchaguzi kuwa ni Kimandolu (Halmashauri ya Jiji la Arusha), Kihesa (Manispaa ya Iringa), Bukumbi (Uyui), Kurui (Kisarawe), Keza (Ngara) na Kwagunda (Korogwe).

Amesema utoaji fomu za uteuzi katika majimbo hayo na kata hizo sita zitatolewa kati ya tarehe 12 hadi 18 Desemba 2017.

Katika jimbo la Songea Mjini utoaji fomu utakuwa kati ya tarehe 14 hadi 20 Desemba mwaka huu. Kampeni zitaanza 21 Desemba 2017 na uchaguzi utakuwa 13 Januari, 2018.

Amesema, katika majimbo ya Singida Kaskazini na Longido, kampeni zake zitaanza pamoa na kata zote sita, tarehe 19 Desemba 2017 na kumalizika 12 Januari.

error: Content is protected !!