August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Visiwa vilivyokuwa giza toka Uhuru, kupata umeme

Baadhi ya nyumba za wakazi wa Kisiwa cha Ukelewe

Spread the love

VISIWA vinne kati ya 38 vilivyopo Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, vitaanza kupata umeme wa nishati ya jua baada ya Kampuni ya Rex Energy kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa umeme kwenye visiwa hivyo, utakaogharimu kiasi cha Sh. 6.5 bilioni, anaandika Moses Mseti.

Visiwa hivyo vinne vyenye watu zaidi ya 40, 600, vitaondokana na tatizo la giza ambalo lilikuwa likisababisha kuwepo kwa matukio ya uhalifu kwa muda mrefu tangu nchi inapata uhuru mwaka 1964 na kuhatarisha maisha ya wananchi hao.

Kampuni hiyo ilioanza utekelezaji mradi huo wa umeme, awamu ya kwanza katika visiwa vya Gana (nyumba 1, 250 na wafanyabiashara 150), Kamasi (nyumba 1, 400 na wafanyabiashara 100), Bwiro (nyumba 2, 500 na wafanyabiashara 150) na kisiwa cha Bulubi chenye (nyumba 500 na wafanyabiashara 50) utaendelea katika visiwa vingine sita wilayani humo.

Hayo yamesemwa leo na Mhandisi Francis Kibhisa, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, mbele ya Frank Bahati, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe wakati wa uzinduzi na kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi huo.

Amesema kuwa mradi huo utasaidia wakazi wa visiwa hivyo kupiga hatua ya kimaendeleo na kuondokana na matumizi ya jenereta wanayotumia kwa gharama kubwa huku akidai umeme huo ni moja ya juhudi za serikali kufikia Tanzania ya viwanda.

Mhandisi Kibhisa amesema kuwa mradi huo wa umeme awamu ya kwanza unaoanza kutekelezwa katika visiwa hivyo vinne na ulioanza kufanyiwa upembuzi yakinufu Februari mwaka jana, utaghalimu kiasi cha Sh. 6.5 bilioni na awamu ya pili ya mradi huo utakaotekelezwa katika visiwa sita utagharimu Sh. 14.6 bilioni.

“Awamu ya pili tutatekeleza katika visiwa sita ambavyo ni Kwetu Juu, Kweru Mto, Izinga, Zeru, Bushengele na Sizu na hiyo yote ni kuunga mkono juhudi za serikali kupitia sekta binafsi, kuhakikisha Tanzania ya viwanda inafanikiwa kwa kuhakikisha nishati ya umeme inapatika ya uhakika,” amesema Mhandisi Kibhisa.

Hata hivyo, amesema kuwa pamoja na kuanza kutekeleza mradi huo wa awamu ya kwanza wa visiwa vinne na utakaokamilika Desemba mwaka huu, pia alidai katika kila kisiwa watakachopita watasaidia serikali katika shughuli za maendeleo ikiwemo afya (kujenga kituo cha afya), elimu, kujenga visima vya maji safi na salama.

“Katika visiwa vinne tunavyoanza kutekeleza mradi huu, tutatumia Sh. 200 milioni na kila sehemu tutakapopita kuwekeza tutatumia kama Sh. 2 bilioni na hiyo kuwaonesha wananchi hatujaja kunufaika sisi pekee na wao wanufaike na sehemu ya miradi hiyo,” amesema Mhandisi Kibhisa ambaye ni mwanzilishi wa kampuni hiyo.

Frank Bahati, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo amesema kuwa, kampuni hiyo itasaidia wafanyabiashara na wananchi wa visiwa hivyo kuwekeza katika miradi mbalimbali ikiwemo ya kuanzisha viwanda vya kusindika samaki, kitendo ambacho kitasaidia kuongeza pato la taifa.

Wakazi wa visiwa hivyo, waliishukru kampuni hiyo kwa kwenda kuwekeza katika visiwa hivyo huku wakidai kwamba itakuwa mkombozi kwao kuondokana na tatizo la giza nyakati za usiku na kuanzisha hata uuzaji wa barufu.

error: Content is protected !!