August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vipers wavuruga Siku ya Mwananchi, waitandika Yanga 2-0

Spread the love

MABINGWA wa Uganda, Vipers SC wamevuruga sherehe za kilele cha Siku ya Wananchi – Yanga S.C baada ya kuwaadhibu kwa bao 2 -0 katika mchezo uliopigwa leo katika dimba la Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mchezo huo uliopigwa leo tarehe 6 Agosti, 2022 umeshuhudiwa na maelfu wa mashabiki waliofurika katika uwanja huo huku walioongozwa na mgeni rasmi katika kilele cha sherehe hizo, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Vipers walianza kuandika bao la kwanza dakika ya kwanza ya mchezo huo kwa bao shuti kali lililopigwa na mchezaji Milton Karisa baada ya kunasa mpira pasi iliyokuwa ikitolewa na beki wa Yanga.

Hadi timu hizo zinakwenda katika vyumba vya mapumziko, Yanga walikuwa nyuma kwa bao moja kwa bila.

Kipindi cha pili Yanga waliingia tofauti kwa kuanza kubadilisha jezi walizozivaa kipindi cha kwanza pamoja na kubadilisha wachezaji sita.

Wakati Yanga wakipambana kufungua safu ya ulinzi ya Viper iliyokuwa ngumu mithili ya kisiki katika mechi hiyo, walipigwa bao la pili lililowaacha vinywa wazi katika dakika ya 64.

Bao hilo lililozima nguvu za Yanga, lilitokana na kona iliyochongwa na Anukani Bright ambapo ilitua moja kwa moja kwenye angle ya mwisho ya mlingoti mitatu ya Yanga na kuandika bao la pili kwa wageni hao.

Yanga waliendelea kulisakama lango la Vipers lakini safu ya ulinzi ya timu hiyo ilionekana kuwa imara na kuwafanya washambuliaji wa Yanga kushindwa kufua dafu mbele ya majogoo hao wa Uganda.

error: Content is protected !!