MTANDAO wa Viongozi Wanawake Barani Afrika (AWLN), umemshauri Rais Samia Suluhu Hassan, azitumie fursa za maendeleo zinazotolewa na taasisi pamoja na mashirika ya kimataifa. Anaripoti Bupe Mwakiteleko, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa tarehe 23 Mei 2021 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Gerson Msigwa, imeeleza kuwa ushauri huo ulitolewa katika mkutano wa viongozi hao, uliofanyika kwa njia ya mtandao jana.
“Katika majadiliano hayo, viongozi wamemueleza Rais Samia, fursa mbalimbali zilizopo katika mashirika na taasisi za kimataifa.
“Fursa hizo, ni pamoja na ufadhili wa fedha, teknolojia na ujuzi kwa ajili ya maendeleo ya nchi mbalimbali duniani,” ameeleza Msigwa katika taarifa hiyo.
Amesema, “wamemshauri kutumia fursa hizo, ili kutimiza malengo yake ya kuiongoza Tanzania.”
Aidha, viongozi hao wamempongeza Rais Samia, kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, akichukua mikoba ya Dk. John Magufuli, aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021.
Samia aliyekuwa Makamu wa Rais, aliapishwa kuwa mrithi wa Dk. Magufuli, tarehe 19 Machi 2021, siku mbili baada ya kifo cha mtangulizi wake huyo.
Dk. Magufuli alifariki dunia, katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya Msigwa ilisema, viongozi hao wanawake barani Afrika, wamemuahidi ushirikiano Rais Samia katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuiongoza Tanzania, ikiwemo kwenye mapambano dhidi ya janga la virusi vya corona.
“Viongozi hao wamemuahidi ushirikiano wowote atakaouhitaji katika uongozi wake, kwenye masuala mbalimbali yakiwemo maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii, haki za wanawake, amani na usalama wa kikanda na janga la ugonjwa wa Korona (Covid-19),” ilisema taarifa ya Msigwa.
Kwa upande wake Rais Samia, aliwashukuru viongozi hao kwa majadiliano waliyoyafanya na ushauri walioutoa kwake, huku akiahidi kushirikiana nao.
Vilevile, Rais Samia aliahidi kushirikiana na taasisi mashirika mbalimbali ya kimataifa, katika kufanikisha jukumu la kuipeleka mbele Tanzania.
Taarifa hiyo imesema, “ameahidi kuendelea kuwapa nafasi za uongozi wanawake wengi zaidi, katika Serikali anayoiongoza ili kufikia lengo la 50 kwa 50, kuimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii zikiwemo afya, maji, elimu na miundombinu.”
“Kama inavyoelekezwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano na kuendelea kupunguza vifo vya akina mama wakati wa kujifungua,” imeeleza taarifa hiyo ya Msigwa.
Wakati huo huo, Rais Samia alisema, ataongeza juhudi katika kukabiliana na changamoto za mazingira ambazo zinapunguza mvua na uzalishaji wa mazao sambamba na Kuweka uwazi katika matumizi ya fedha za umma na kuongeza juhudi za kukabiliana na covid-19.
Nimefurahi kushiriki na viongozi wenzangu katika mkutano wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Barani Afrika (African Women Leaders Network-AWLN) uliofanyika kwa njia ya mtandao. Nimewaeleza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuwaletea Watanzania maendeleo na wameahidi kuniunga mkono
— Samia Suluhu (@SuluhuSamia) May 23, 2021
Alisema, “Rais Samia ametoa wito kwa washirika mbalimbali wa maendeleo, kuongeza ushirikiano na Tanzania. Pia amewaomba viongozi hao kuendelea kujadiliana na kubadilishana mawazo mara kwa mara, juu ya kulisaidia Bara la Afrika kupiga hatua za kimaendeleo na kuinua zaidi ustawi wa jamii hasa wanawake na watoto ambao wanakabiliwa na madhara ya changamoto nyingi.”
Taarifa ya Msigwa ilisema, mkutano huo wa AWLN uliitishwa na Rais Mstaafu wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, kwa lengo la kubadilisha uzoefu wa uongozi na kupeana taarifa juu ya fursa mbalimbali.
Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo, ni pamoja na Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ethiopia Sahle-Work Zewde.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohamed. Rais mstaafu wa Jamhuri ya Malawi, Joyce Banda na Rais mstaafu wa serikali ya mpito ya Jamhuri ya Afrika Kati, Catherine Samba-Panza.
Wengine, ni rais mstaafu wa Jamhuri ya Mauritius, Ameena Gurib-Fakim.
Mwanzilishi wa AWLN Tanzania na Katibu mkuu wa mkutano wa nne wa wanawake duniani, Getrude Mongella. Pamoja na Mjumbe Maalum wa Afrika katika masuala ya amani na usalama, Dk. Bineta Diop.
Leave a comment