Friday , 3 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Viongozi wa siasa, dini, wanasheria wakataa subira ya Rais Samia
Habari za SiasaTangulizi

Viongozi wa siasa, dini, wanasheria wakataa subira ya Rais Samia

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan
Spread the love

 

KAULI ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuweka kiporo suala la Katiba Mpya na kuendeleza zuio la mikutano ya hadhara ili afufue kwanza uchumi, imeleta balaa na kuibua mjadala mzito nchini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mjadala huo umeibuka miongoni mwa wananchi, viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani, ambao wengi wanapingana na msimamo wa Rais Samia, huku wengine wakieleza kuvunjika nyoyo.

Mbali ya viongozi wa siasa, mjadala huo pia umetikisa baadhi ya viongozi wa dini, wanasheria na wanaharakati, ambao wamemsihi Rais Samia kutupia jicho Katiba Mpya, kurejesha shughuli za kisiasa na kukutana na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani, mapema iwezekanavyo.

Katika mkutano wake Jumatatu iliyopita ya tarehe 28 Juni 2021, Ikulu ya Dar es Salaam alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari, Rais Samia aliahidi kushughulikia madai ya Katiba Mpya, lakini akaomba muda kidogo ambao hakuutaja, ili afufue kwanza uchumi na kuuweka katika hali mzuri.

“Naomba nipeni muda nisimamishe nchi kwanza kiuchumi, tuite wawekezaji, ajira zipatikane, uchumi ufunguke, halafu tutashughulikia mengine,tutashughulikia Katiba, tutashughulikia hiyo mikutano ya hadhara wakati ukifika,” alisema Rais Samia.

Mbali na ahadi ya Katiba, Rais Samia pia alisema hata suala la kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani kama alivyoahidi Dodoma, nalo lisubiri kidogo ili ajikite kwenye kufufua uchumi na kukabiliana na changamoto zinazolikabili Taifa kwa sasa.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe aliandika katika ukurasa wake wa Twitter, kuwa katika hili ‘Mama hapana!’

“Mama, Mama, Mama, kwenye hili hapana! Yawezekana wewe na washauri wako, hamjaelewa maumivu tuliyopitia kwa miaka mitano ya mtangulizi wako. Na ndiyo sababu tulikuomba sana utusikilize mapema. Kauli hii leo, umetulaza na machozi, very, very sad (inasikitisha sana, sana).

Kabla ya andiko hili, hivi karibuni Mbowe akiwa kwenye mikutano yake ya ndani mikoani, aliendelea kumsihi Rais Samia akutane na wapinzani, ili pamoja na mambo mengine, watibu madonda yaliyotokana na mnyukano wa uchaguzi mkuu uliopita.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

“Kuna watu tumeumizwa sana na utawala uliopita, baadhi yetu wamelazimika kukimbia nchi kuhofia maisha yao, wapo wenzetu wanaozea jela kwa kesi za kubambikizwa, na wengine kupoteza maisha, hayo yote tunataka kuonana na Rais Samia ili tuanze upya, Taifa likiwa na umoja na mshikamano wa pamoja,” alisema Mbowe.

Pamoja na Chadema kumwandikia barua Rais Samia na kuomba kukutana naye nay eye kukubali, lakini Jumatatu iliyopita, alizima ndoto zao kwenye mkutano wa Ikulu na wahariri.

Zitto Kabwe

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alipoombwa kutoa maoni yake juu ya msimamo wa Rais Samia, alijibu kwa ufupi tu kuwa: “Nimevunjika moyo.’

Hata hivyo, ACT-Wazalendo baadaye ilitoa taarifa kuhusu msimamo wa Rais Samia, ikisema imepokea kwa masikitiko makubwa kauli ya Rais, kwamba mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na Katiba mpya, visubiri asimamishe nchi na kujenga uchumi wa Taifa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kauli hiyo aliyoitoa akizungumza na wahariri kuadhimisha siku 100 za utawala wake, ni mwiba unaowachoma wapenda demokrasia, watetezi wa haki za binadamu na Watanzania kwa ujumla.

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo

“Kuhusu Katiba mpya, ACT tuna matumaini, kwamba ni msingi na kichocheo cha maendeleo, hakuna maendeleo ya uhakika yanayoweza kupatikana bila kwanza kuweka msingi madhubuti wa kikatiba.”

“CCM ambayo imekuwa madarakani tangu Uhuru, haiwezi kuwakosesha wananchi haki yao ya kupata Katiba Mpya kwa kisingizio cha kujenga uchumi wa nchi,” ilisema taarifa hiyo.

Kuhusu mikutano, taarifa hiyo ilisema ni haki inayolindwa na Katiba na sheria. “Katiba ya Tanzania (Ibara ya 3) na Sheria ya vyama vya siasa (Kifungu cha 11), vinatoa haki ya vyama vya siasa, kukusanyika.

“Rais wa nchi ambaye ameapa kuilinda na kuitetea Katiba na sheria za nchi, hapaswi kuzuia haki ambayo imetolewa na kulindwa na sheria,” ilisema ACT.

ACT-Wazalendo ilitoa mwito kwa Rais Samia, atafakari upya msimamo wake kuhusu Katiba mpya, na haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.

“Iwapo ataendelea na msimamo huo, bila shaka atakuwa ameutia doa kubwa utawala wake, na kupanda mbegu itakayolirudisha nyuma na kuligawa Taifa,” ilisema taarifa hiyo.

James Mbatia

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ni miongoni mwa wanasiasa waliotoa maoni yao kuhusu kauli ya Rais Samia.

Alisema kuahirisha mchakato wa Katiba kwa kisingizio cha kujenga uchumi kwanza, ni kutolitendea haki Taifa.

“Kauli za Rais Samia ni tofauti na matendo yake, alipozungumza na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), alisema atalinda na kuitetea Katiba, hii Katiba si yake, ni mali ya wananchi,” alisema na kuongeza:

“Rais asitake tutunishiane misuli, ajitafakari upya, mimi nampa tahadhari, nchi ina chuki na hasira sana, nchi imevimba, nchi imeonewa sana na utawala wa CCM, kwa kutumia Katiba hii ya sasa, dawa ya hayo yote ni Katiba Mpya,” alisema Mbatia.

Kiongozi huyo alimtaka Rais Samia kurejea historia ya Taifa la Libya, kwamba licha ya kuwa na uchumi mzuri, wananchi wake walikosa uhuru wao wa kikatiba, mwishowe waliwaondoa watawala wao kwa aibu.

Alisema anaamini siasa na uchumi vinakwenda pamoja, hivyo haiwezekani kukuza uchumi kwa kuweka kiporo Katiba mpya.

“Rais Samia ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, atambue kuwa chama chake kiliharibu uchaguzi mwaka jana, kwa sababu ya Katiba mbovu, hatuna muda tena wa kusubiri. Ili utawala wake uheshimike, azingatie utawala wa sheria,” alisema Mbatia.

Jebra Kambole

Mwanasheria maarufu nchini humo, Jebra Kambole, akizungumzia msimamo wa Rais Samia, alisema: “Huwezi kujenga uchumi bila utawala bora, na huwezi kuwa na utawala bora bila utawala wa sheria, na huwezi kuwa na utawala wa sheria kama hauheshimu haki za binadamu na uhuru wa mahakama, na huwezi kupata hivyo, bila Katiba bora, hii ya sasa si bora, tunataka mpya.”

Askofu Mwamakula

Askofu wa Kanisa la Uamsho la Moravian, Emmaus Mwamakula, akitoa maoni yake, alisema: “wawekezaji na demokrasia ni sawa mtoto na mbeleko, ikikatika mbeleko, mtoto huanguka.

“Ukiminya demokrasia wawekezaji hukimbia, huwezi kumnyima pumzi mjamzito, ukatarajia mtoto aliye tumboni ataendelea kuishi. Muujiza wa aina hiyo haujatendeka katika uso wa dunia.

Emmaus Mwamakula

Askofu Bagonza

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, alisema ni hatari kuahirisha matumizi ya sheria na Katiba katika kuongoza nchi kwa sababu yoyote.

Alisema tawala za kijeshi ndizo zenye tabia hii, na tawala za kiraia huweza kufanya hivyo wakati wa vita, au hali ya hatari kwa ruhusa maalumu ya Bunge.

Askofu Bagonza aliongeza kuwa Taifa limewahi kushuhudia zuio la Serikali la mikutano ya kisiasa ya hadhara, ili kwanza kunyoosha nchi.

“Tumeshuhudia zuio la nyongeza ya mishahara, ili kwanza kukamilisha miradi ya kimkakati, zuio la upandishaji madaraja na vyeo kazini, ili kwanza tuhakiki mambo,” alisema Askofu Bagonza.

Askofu Benson Kagonza, KKKT Dayosisi ya Karagwe

Kwa mujibu wa Askofu Bagonza, Taifa lilishuhudia pia kukamata watu na kuwaweka ndani bila utaratibu, kwa maelezo kuwa nchi iko kwenye vita ya kiuchumi na huko nyuma “tumepigwa sana”.

Aliasa kuwa Serikali inapoanza kuahirisha matumizi ya Katiba au sheria, inakuwa imekabidhi nchi iongozwe na mtu au kundi na hatari zake zinajulikana.

Alizitaja athari hizo kuwa ni pamoja na wawekezaji kushindwa kukuamini, kwa sababu hawajui kesho itaamuliwa nini, kwani usalama wa mitaji yao huletwa na sheria na si matamshi wala ahadi.

“Kuweka nchi sawa kwanza” ni kazi isiyokwisha na ni ya kila siku. Nchi huwekwa sawa, kwa kutumia Katiba na sheria si kwa kuahirisha matumizi ya Katiba na sheria,” alisema.

“Aliyepita alifanya mambo. Huyu amefanya mambo kwa siku 100 yakafurahisha. Akija mwingine kwa mazingira ya alivyokuja huyu (hatuombei), naye aondoe haya na kuleta mengine? Tutamaliza lini?” Alihoji Dk. Bagonza.

Askofu huyo alisema uhuru wa kisiasa ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi, hivyo ukiahirisha maisha ya siasa, umesimamisha ukuaji wa uchumi.

Alisema haki na uhuru ni misingi imara ya kuweka nchi sawa, lakini ukiyaahirisha unajitwisha mzigo mzito.

“Dai la Katiba mpya lina faida kubwa kwa Rais, kuliko kwa taasisi nyinginezo. Katiba mpya ni dawa si kikwazo. Nampongeza mama kwa ‘100 kwanza’. Namwombea ‘100 tena’ zenye maono mapana zaidi.

Msimamo wa Samia

Akijibu swali la mmoja wa wahariri aliyetaka kujua lini atakutana na wapinzani na hatima ya zuio la mikutano ya hadhara na mchakato wa Katiba Mpya, Rais Samia aliwasihi wananchi na wanasiasa, kuwa na subira kuhusu mchakato wa Katiba mpya na mikutano ya siasa ya hadhara.

Rais Samia ambaye ametimiza siku 100 tangu alipoingia madarakani, tarehe 19 Machi 2021, alisisitiza kuomba wananchi kumuunga mkono katika harakati zake za kufufua za uchumi.

Akijibu swali la mmoja wa wahariri aliyetaka kujua lini atakutana na wapinzani na hatima ya zuio la mikutano ya hadhara na mchakato wa Katiba mpya, Rais Samia aliwasihi wananchi na wanasiasa kuvuta subira, kuhusu mchakato wa Katiba Mpya na mikutano ya siasa ya hadhara.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

“Kwa sasa tumeruhusu mikutano ya ndani ya siasa, wabunge kwenye maeneo yao, lakini si mbunge atoke eneo lake, aende kwingine, lakini ile ya hadhara tujipe muda.”

Akigusia Katiba mpya, Rais Samia alisema: “Sisemi Katiba mpya si ya maana, hapana nipeni muda kwanza tujijenge kiuchumi.”

Kiongozi huyo wa nchi aliingia madarakani tarehe 19 Machi 2021, baada ya kifo cha mtangulizi wake, Dk John Magufuli, kilichotokea Machi 17 Dar es Salaam.

“Siku 100 za uongozi wako, Rais tumeona unasimamia haki, uhuru, demokrasia na utawala bora, kumekuwa na swali linaulizwaulizwa, lakini hatujapata kauli yako, kuwa Rais anasema nini,” aliuliza Steven Chuwa, Mhariri wa ITV na Radio One.

Pia, mwakilishi wa Idhaa ya Ujerumani (DW), Hawa Bihoga aliuliza “kulikuwa na tamko la marufuku ya mikutano ya kisiasa, lakini sasa umetimiza miaka 100 madarakani, ni lini sasa utatoa tamko ili mikutano iwe rasmi na ni lini utakutana na viongozi wa upinzani kama ulivyoahidi utakutana nao?”

Akijibu maswali hayo, Rais Samia alisema: “Kuna mambo mengi tunataka kuyashughulikia, nimesema nakwenda kuifungua nchi, uchumi umeshuka, tunataka kuupandisha.

“Tukifungua nchi na kwenda kuiweka vizuri, wawekezaji waliosajiliwa kipindi kama hiki Machi hadi sasa, ni mara mbili ukilinganisha na mwaka jana,” alisema.

Alisema: “Wawekezaji wanazidi kuja na ninapofungua milango ya uchumi, lengo langu wawekezaji wakubwa waje, fedha zizunguke mifukoni, tukusanye mapato, tukusanye kodi nyingi na hilo linataka nchi iwe na amani na utulivu, na nchi iwe inakwenda vizuri.

“Sasa katika kufanya hivyo, ni jukumu la kila mmoja, uchumi ukipanda, unapanda kwa kila mmoja, kila mmoja atapata ajira, tutaacha kulalamika,” alisema.

“Nawaomba sana Watanzania kama mnavyosema, nimeanza vizuri, nipeni muda niisimamishe nchi kiuchumi, halafu tutashughulikia mengine kama Katiba na kukutana na vyama vya siasa,” alisema Rais Samia.

1 Comment

  • Hayo yote ni yakidunia tuyajua na wala sio ajabu ya kizunguzwa ktk kampeni ya uchaguzi mkuu ccm haikunad katiba mpya imenadani mafaniiko na maendeleo na ikaidi kutatua kero za wananchi ndipo hapo wananchi wakaipa ushind ccm .na vile vyama vilivyo nadi katiba na serekari wananchi wamenyima ushind sasa mnataka katiba mpya kutoka mamlaka gani unaposema viongozi wadi wanataka katiba mpya kutoka mamlaka gani ikiwa umma umekichagua chama cha ccm ambacho katika ilani yake aikuzungumzia katiba mpya tusubiri 2025.vyama vinadi katiba mpya na mikutono ya hadhara tuone kama vitapA tiketi ya kufika dodoma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Vijana ACT-Wazalendo Dar wampa tano Rais Samia

Spread the love  NGOME ya Vijana ya Chama cha ACT-Wazalendo, kimempongeza Rais...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yaiangukia Serikali kunusuru wananchi Liwale, Nachingwea

Spread the love  CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimeitaka Serikali kuchukua hatua za haraka...

Habari za SiasaTangulizi

Vigogo wanaokwamisha mradi Liganga na Mchuchuma kitanzani

Spread the love  NAIBU Spika wa Bunge, Mussa Zungu, watu wanaokwamisha utekelezaji...

Habari za Siasa

Gridi ya Taifa kufumuliwa kukabiliana na katizo la mgao wa umeme

Spread the love  WAZIRI wa Nishati, Januari Makamba, amesema Serikali ina mpango...

error: Content is protected !!