July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Viongozi wa Kiislam walalamika kuteswa

Watuhumiwa na kesi ya ugaidi wakifikishwa katika Mahakama ya Kisutu

Spread the love

SERIKALI ya Rais Jakaya Kikwete imeingia katika kashfa nzito ya askari wake kutajwa kuwa wanaendesha mateso kwa watuhumiwa wanaokuwa kwneye mamlaka ya Jeshi la Polisi.

Kashfa hiyo imethibitika wiki iliyopita wakati mmoja wa viongozi wakuu wa asasi ya Kiislam ya Uamsho ya Zanzibar, Sheikh Farid Ahmed Hadi, alipolalamika kuwa waliteswa na kudhalilishwa kijinsia wakiwa mikononi mwa Polisi.

Sheikh Farid ambaye ameunganishwa katika kesi ya jinai ya tuhuma za kutenda vitendo vya ugaidi inayowakabili maulamaa wengine 21, aliiambia mahakama kuwa baadhi yao walipigwa sana na askari hadi kuvuja damu na hawakupelekwa hospitali.

Alieleza kuwa waliomba kuruhusiwa kwenda hospitali kwa ajili ya matibabu lakini hakuna aliyewajali badala yake walikuwa wakipewa kauli za kejeli na kudhalilishwa kwa maneno ya ovyo.

Sheikh Farid alitoa maelezo hayo baada ya kupewa nafasi na Hakimu Heleen Liwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni katika kutimiza ahadi ambayo hakimu huyo alitoa wiki mbili kabla, aliposema angewapa nafasi kueleza malalamiko yao pale kesi itakapoitishwa tena kwa kutajwa.

Awali, Sheikh Farid aliijulisha mahakama kuhusu mateso na udhalilishaji walipofikishwa mahakamani Agosti 6 na 21 mwaka huu.

Alidai wanaishi vizuri gerezani kwa kufuata sheria isipokuwa suala la matibabu hawajatimiziwa ipasavyo kutokana na kuelezwa kuwa hospitali ya gereza haina bajeti ya kutosha. Wameruhusiwa kuagiza dawa nje hatua ambayo si ya haki.

“Watu wameingia gerezani wanaumwa, wanavuja hadi usaha kutokana na kipigo walichopewa na polisi lakini hawajatibiwa. Ni unyama mkubwa ambao tunamuomba Rais auchukulie hatua kwa kuunda tume ya kutufanyia uchunguzi afya zetu,” alieleza mahakamani.

“Sisi tunachodai siyo uchochezi. Ninayaeleza haya na polisi wapo wameyasikia kwamba tumekamatwa na kushtakiwa Tanganyika kwani Zanzibar siyo nchi kwanini tusishitakiwe kule nyumbani waliko ndugu zetu,” alihoji.

Kuhusu malalamiko ya kuwa wangeshitakiwa Zanzibar, Hakimu Liwa alisema anachojua ni kwamba watuhumiwa wote ni raia wa Tanzania na “suala la Muungano wengine wanauamini na wengine wanataka ukazikwe Butiama.”

Masheikh na maulamaa 22 walikamatwa Zanzibar, Dar es Salaam na Arusha vipindi tofauti na kusafirishwa kwa njia ya anga na bahari (kwa wale waliokamatwa Zanzibar) na kufunguliwa mashitaka ya kushiriki vitendo vya kigaidi.

Kesi hiyo pia inawakabili masheikh Mselem Ali Mselem na Abdalla Said Ali (Madawa) ambao pia ni viongozi wakuu wa Uamsho, taasisi ambayo imekumbwa na kadhia ya kutuhumiwa kuhusika na vitendo vya fujo.

Sheikh Farid alielekezwa kuyaandika malalamiko yao ili yakabidhiwe kunakohusika ili yafanyiwe kazi. Kesi yao iliahirishwa hadi itakapotajwa tena 17 Septemba 2014. Watuhumiwa wote wako rumande kwa kuwa kesi hiyo ipo katika hatua ya uchunguzi.

Mashitaka dhidi yao yamefunguliwa chini ya Sheria ya Kudhibiti Ugaida, Na. 2 ya mwaka 2002 iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano mwaka 2002, miezi michache baada ya magaidi kushambulia majengo muhimu yalioko nchini Marekani.

Majengo hayo ni Pentagon ambalo ni makao makuu ya Wizara ya Ulinzi jijini Washington, na Kituo cha Kimataifa cha Biashara – World Trade Centre (WTC) kilichopo jijini New York. Mashambulizi hayo yaliyofanywa kwa kutumia ndege za abiria, yalifanywa wakati mmoja 11 Septemba, 2001.

Wiki iliyopita, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambayo ni asasi ya serikali, ilitoa taarifa ya kuwepo kwa malalamiko mengi ya watuhumiwa wa makosa ya jinai kuteswa na kudhalilishwa wakati wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola.

error: Content is protected !!