January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Viongozi wa dini: Wezi wa kura wasulubiwe

Spread the love

WATANZANIA wanaofuata zaidi dini mbili kuu za Kiislam na Kikristo, leo walishiriki kuitika dua zilizotolewa na viongozi wao wakati wa mkutano wa uzinduzi wa kampeni ya mgombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Viongozi walioomba dua ni Sheikh Said Rico, ulamaa wa Kiislam anayeishi jijini Arusha ambaye alialikwa rasmi katika uzinduzi huo, na kiongozi wa Kikristo aliyesoma dua kwa upande wa dini hiyo, ni Askofu Josephat Gwajima, rafiki mkubwa wa Edward Lowassa.

Katika dua zao, wote wawili waliomba kwa Mwenyezi Mungu awasulubu wezi watakaoshiriki kuiba kura za wagombea wa UKAWA. Lowassa anafuatana na Juma Duni Haji, ambaye ndiye mgombea mwenza wake.

“Tunamuomba Mwenyezi Mungu, msimamizi wa haki, kwamba mtu yeyote atakayeiba kura zetu au kufanya ulaghai wowote apate kansa ya damu, mirija ya mikojo uizibe,” amesema Sheikh Rico katika dua iliyoitikiwa kwa nguvu kubwa na umma wa wananchi waliohudhuria mkutano huo kwenye viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam.

Akisoma dua jukwaani, Askofu Gwajima aliwema, “Majira hayawafuati watu, watu hufuata majira; muda huu ni muda wa mabadiliko tunakuomba Bwana utufanyie Lowassa kuwa ndio Josho letu, uwaangamize wanaopinga haki kama ulivyowaangamiza waliopinga watu wake.”

Askofu Gwajima alisema Mungu ataweka mkono wake kwa Lowassa ambaye baadhi ya watu wasiomtakia mema, wanamtabiria mabaya.

Viongozi hao walipanda jukwaani kuomba dua baada ya muongoza mkutano, John Mrema, ambaye ni mkurugenzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) anayeshughulikia masuala ya Bunge, kusema:

“Tunaanza na Mungu na tunamaliza na Mungu.’’ Mrema aliongoza mkutano huo uliohudhuriwa na umma wa wananchi wakiwemo wafuasi wa Chadema, pamoja na vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).

error: Content is protected !!