December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Viongozi wa dini wataja sababu kumpa Samia tuzo

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

JUMUIYA ya Maridhiano Mkoa wa Mbeya imesema mojawapo ya sababu za kumpa tuzo ya heshima Rais Samia Suluhu Hassan ni kutokana na jitihada zake za kudumisha amani pamoja na utawala bora aliouonesha tangu alipoingia madarakani Machi 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya … (endelea).

Pia uboreshaji wa huduma za elimu pamoja na ufuatiliaji wa miradi ni moja ya mambo yaliyowasukuma viongozi hao wa dini kumpatia tuzo hiyo ya heshima.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 17 Novemba, 2022 jijini Mbeya na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Mkoa wa Mbeya, Askofu Oscar Ongere wakati akizungumza katika hafla ya kukabidhi tuzo ya heshima kwa Rais Samia pamoja na kuliombea taifa.

Askofu Ongere amesema jicho la Rais Samia limetembea katika sehemu mbalimbali nchini kuhakikisha kwamba Tanzania inaendelea kuwa na amani.

“Kwanza kilichofanya mimi na timu yetu kufanya tukio hilo ni juhudi za Rais Samia kudumisha amani na utulivu ambao toka ameingia madarakani kila mmoja kwa jicho lake ameona kuna utulivu.

“Pili tumeona kitu kinaitwa utawala bora. Tumeona katika nafasi zote za uongozi lakini pia katika maamuzi mambo mazuri yameendelea kufanyika ndani ya Taifa letu. Kwa sababu hiyo ametoa fursa kwa kada zote vijana, wa-baba na wa-mama. Taifa linakwenda vizuri.

“Tumeona akithamini sana viongozi wa dini, amekuwa akiwatembelea hata kwenye madhehebu yao na ameshikana bega kwa bega bila kujajali dini kabila wala rangi,” amesema.

Aidha, kingine amesema Rais Samia amekuwa akifuatilia miradi mbalimbali hasa ikizingatiwa nchi haiwezi kuendelea bila kuwa na miundombinu mizuri ikiwamo afya.

“Mama amejali sana maisha ya watanzania, tumekuja kusema asante na kumtia moyo. Mtu anapofanya vizuri na kujitoa kwa ajili yetu inatupasa kusema asante,” amesema.

Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Msafiri Njalambaha amesema Rais Samia amedhihirisha utumishi wake kwa Watanzania kwa kuboresha upatikanaji wa elimu kwa Watanzania.

“Amejenga madarasa mengi nchi nzima… fedha za mkopo utokanao na UVIKO- 19 amezitumia kwa uadilifu na sasa zimefika kila sehemu. Madarasa yalikuwa machache lakini ameondosha hilo… Mbeya tumepata fedha nyingi. Sote tunashuhudia na kusikia ndio maana tumeona tumpe nishani Mama,” amesema.

Akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Rais Samia, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera mbali na kuwashukuru viongozi hao wa dini kwa niaba ya rais, amesema mambo mengi aliyoyafanya mkuu huyo wa nchi amedhihirisha kuwa anipenda Mbeya.

“Yote yanayokuja ndani ya Mbeya hayaji kwa bahati mbaya… aliwaletea Spika wa Bunge, uwanja wa ndege Songwe pamoja na jengo la abiria na sasa ndege zinatua usiku ndani ya Mbeya ikiwa ndege kubwa ya Boeing air bus.

“Ndio maana viongozi wa dini wameguswa. Tuzo nitaifikisha kwa Rais kwa sababu jana aliniambia kutokana na maandalizi ya hafla hii, alisema viongozi wa dini wamempa nguvu kufanya makubwa zaidi ndani ya mkoa wa Mbeya,” amesema.

Aidha, ametoa wito kwa watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Samia bila manung’uniko ikiwa ni pamoja na kuendelea kufanya kazi kwa bidi.

“Tuache itikadi zetu za dini, siasa tuende na Samia. Sisi ndio machawa wake wa kueleza ukweli, wasiokuwa na masikio tutawazibua,” amesema.

error: Content is protected !!