ASKOFU wa Kanisa la Power of God lililopo eneo la Chanika, Dankon Rwaikila amewaomba watumishi wa dini kumuomba Mungu ili atuchagulie viongozi wenye hofu ya Mungu watakaoweza kujitoa katika nchi yetu ambao wataleta maendeleo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza hayo jana Jumapili tarehe 28 Juni 2020 wakati wa ibada maalumu kwa ajili ya kuwaombea wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari ambapo shule zimefunguliwa leo Jumatatu.
Rwaikila amesema watumishi hao wa dini watakapokuwa na mshikamano wa kumuomba Mungu taifa litapata viongozi wazalendo ambao wenye hofu ya Mungu watakaoweza kujitoa katika nchi yetu.
Pia, maombi hayo yatasaidia kupata viongozi ambao wataweza kuunga juhudi za Rais John Magufuli watakaoweza kutupeleka kwenye ndoto ya Tanzania mpya.
“Ninachojua, jambo zuri linapotaka kutokea shetani anajiinua, hivyo biblia inasema ukimuomba Mungu atatuepusha na mabaya kwenye nchi yetu atupe mshikamano ili tumalize uchaguzi wetu tukiwa na amani na umoja,”amesema Rwaikila.

Pia, amesema wazazi na walezi waendelee kumwamini Mungu kwa kuwa atawalinda watoto wanapokuwa shuleni na Mungu ataendelea kuliokoa taifa na janga hilo la ugonjwa wa Corona.
Wakati huo huo, Askofu wa Kanisa la Reviral and Praise Fellowship lililopo Chanika, Edmund Kihwili alisema, Mungu ataendelea kuwalinda wanafunzi shuleni kwa kuwa wengi wanahofu wakijua ugonjwa haujaisha hivyo wazazi wanatakiwa wawapeleke watoto wao shuleni.
“Kinachotakiwa kumuamini Mungu na kumthamini, tumeona ushindi na mkono wa bwana umetenda kwa kutuepusha na ugonjwa huu wa Corona,” amesema Kihwili.
Leave a comment