July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Viongozi wa dini wamewasaliti wananchi

Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Donald Mtetemela

Spread the love

KATIKA maandiko matakatifu kwa maana ya Biblia Takatifu alikuwepo nabii aliyeitwa Yohana Mbatizaji. Huyu alikuwa mnyenyekevu, na mpole lakini aliyezungumza kwa sauti kali pale alipokuwa anakemea maovu na kwa watenda maovu.

Aliwakemea na kuwaambia ukweli wote bila kujali cheo cha mtu, na ingawa wengine walimwona kama mtu aliyechanganyikiwa, hakujali wala kuogopa japo ilimpasa hata kufa kwa kuusema ukweli kwa kuwa alikuwa anatimiza wajibu.

Alionekana wa ajabu kutokana na maisha aliyokuwa akiishi, yaliwashangaza wengi. Aliishi porini akila nzige,  asali na matunda ya pori na huku akihubiri habari za ufalme wa Mungu akiwataka watu watubu dhambi zao, kutenda haki, kuwa wakweli, kutodhulumu watu haki zao na kutoa miongozo kwa makundi mbalimbali namna iwapasavyo kuenenda  ili kutimiza mapenzi ya Mungu.

Yohana aliwahi kumkemea Herode kwa kitendo chake cha kumchukua mke wa ndugu yake. Alimkemea bila kujali ufalme wake na majeshi yake yote na nguvu zake zote alizokuwa nazo za kuweza kumfanya chochote.

Nia yangu sio kuhubiri ila kutumia mifano ya kitabu hicho kuwataka wahubiri waishi kadri ya matakwa ya Biblia. Kwa hali ilivyo, sioni wahubiri wanaopaswa kutuonyesha njia ila wanaotupoteza njia na pengine kutuangamiza kabisa sio sisi tu, bali na rasilimali zetu.

Viongozi wetu wa dini zote wametugeuka, wametusaliti na wanaendelea kutusaliti, kutuhujumu, kutuasi, kutudhulumu na sio tena kimbilio la kiroho na kimwili. Nayasema haya kwa uchungu mkubwa sana baada ya tafakuri ndefu kabisa kwani yanayotokea, kwa kweli hayaakisi mategemeo tuliyoweka kwao.

Viongozi wa dini wamekuwa uchochoro wa maovu ya watawala, ni sehemu ya kusemea, na kutenda na kuficha uovu wao na sehemu ya kuhalalisha madhambi yao, huku wanyonge wakitaabika, kudhalilika, kuteseka na kunyanyasika.

Viongozi wa dini wanacheza ngoma ya wanasiasa. Hawana uwezo wa kukemea. Kunguru hawawezi kuruka pamoja na njiwa, na ukiona hivyo kuna sababu. Hali ilivyo, haiwezekani kwa sasa kutenganisha viongozi wa dini na viongozi wa kisiasa kwa matendo yao na kauli zao.

Madhara ya ushirika wa wanasiasa na viongozi wa dini rasilimali zinaondoka, rushwa inakithiri, madini yanachotwa, dawa za kulevya zimetapakaa kila pembe ya nchi au kuwa uchochoro wa kupitisha dawa hizo na hakuna anayekemea.

Maliasili zetu zinatoroshwa katika maeneo ambako kuna wachungaji, mapadri, mashehe na maaskofu lakini hakuna anayekemea! Zinazuka operasheni mbalimbali ambazo zimegharimu maisha ya watu na mali zao kama Operesheni Tokomeza Ujangili lakini hakuna anayekemea.

Watu wananyanyasika katika ardhi yao, maeneo yao hata kuuana baina ya makabila tofauti na kuambiwa watawala wa serekali wamekuwa ni kichocheo cha hiyo migogoro husika lakini hakuna anayekemea.

Viongozi wa dini hawawezi kukosoa viongozi kwa sababu nao si wasafi. Mwaka 2011, Rais Jakaya Kikwete hakumung’unya maneno, aliwataka maaskofu waache kuuza dawa za kulevya. Maaskofu walibisha, lakini siku chache baadaye Jeshi la Polisi lilimkamata mhubiri mmoja kwa tuhuma za kuuza dawa za kulevya. Ndiyo, hakuwa Mtazania, alikuwa Mnigeria, lakini alikuwa mhubiri.

Kama wanajihusisha na uhalifu huo, wanawezaje kuikemea serikali? Viongozi wa dini hawawezi kuikosoa serikali kwa sababu sababu fedha zilizokwapuliwa na mafisadi zinakwenda kwenye nyumba za ibada kama sehemu ya michango ya ujenzi wa makanisa na misikiti. Pia mafisadi wanapotaka kutakatisha fedha hukimbilia kutoa michango ya ujenzi.

Iko mifano mingi kuthibitisha viongozi wa dini waliposhindwa kutimiza wajibu kwa wananchi nchi zilitumbukia kwenye machafuko na miongoni mwao ni nchi jirani zetu kama Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya.

Viongozi wa dini Rwanda walikuwa sehemu ya uchochezi wa kikabila, wakageuka wito wa kiroho. Vita vilipoisha, viongozi wa dini walikuwa miongoni mwa watu walioshitakiwa mahakamani.

Machafuko yalipoibuka nchini Kenya 2007/08 baada ya uchaguzi, kiongozi mmoja wa dini alikuwa sehemu ya machafuko. Afrika Kati ambako kuna machafuko, vita vya kidini; waislamu wakikimbilia makanisani huhatarisha maisha yao; si sehemu salama tena kiroho na kimwili.

Kwa sasa kuna mchakato wa kuandika katiba mpya. Masheikh na maaskofu waliomo ndani ya Bunge Maalum la Katiba, waliposikia wajumbe wakikashifiana, wakitukanana na kudhalilishana walikaa kimya, hawakukemea. Hapo si ndipo walipopaswa kuonesha uwepo wao?

Kwa nini hawakukemea kauli za kejeli, udini, ubaguzi, mipasho, na matusi tena ya nguoni zilizotolewa na wajumbe? Hawakusikia? Au hayakuwahusu? Katika mlango huo wa matusi, wahubiri wetu walipaswa kusimama hapo kwamba hayo si sehemu ya Ibara zinazojadiliwa.

Joto la matusi lilipozidi, wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliamua kutoka. Bunge hilo limeanza vikao vyake bila Ukawa.

Viongozi wa dini wanaothubutu kutaka Ukawa warudi katika mazingira waliyoyaona ni usaliti wa kiroho. Mchungaji mwema ni Yule anayepeleka mifugo yake eneo ambako hakuna samba, fisi wala mbwa mwitu, lakini viongozi wa dini wanahimiza Ukawa warudi eneo ambalo halijabadilika.

Cha ajabu na kusikitisha wale walioharibu hawakemewi wala kutakiwa kuomba radhi kwa matendo yao ila wanaandamwa watetezi wa wananchi. Swali la kuwauliza viongozi wa dini ni nini wajibu wao? Kwa nini wanashindwa kukosoa na kurekebisha jamii?  Je, dini zimeshindwa kukemea maovu au viongozi wa dini wameshindwa kukemea uhalifu? Kwa nini hawana ujasiri kama Papa Francis asiyetetea uhalifu wa kibinadamu?

Nijuavyo, wajibu wa viongozi wa dini ni kuchunga kondoo wa Bwana ili wapate malisho mema kimwili na kiroho kinyume cha hayo ni ubatili. Wasibaki kusoma na kusimulia matendo mema ya Yohana, wafuate.

Makala hii imeandikwa na  Oscar James anapatikana kwa 0769815890 Kabenguli76@gmai.com

error: Content is protected !!