May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Viongozi wa dini wakemea vurugu, kejeli na matusi uchaguzi mkuu 2020

Spread the love

VIONGOZI wa dini nchini Tanzania, wamekemea vitendo vya vurugu kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Salamu hizo zimetolewa leo Jumatatu tarehe 17 Agosti 2020 na Askofu Jackson Sosthenes wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, katika Mkutano wa Viongozi wa Dini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Pia, mkutano huo utaunga mkono juhudi za Rais wa Tanzania, John Magufuli na Serikali yake katika ustawi wa amani, uzalendo na kumtanguliza Mungu na mgeni rasmi ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Mkutano huo umeandaliwa na Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini kutoka mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar.

Akisoma salamu za viongozi hao wa kiroho, Askofu Sosthenes amevitaka vyama vya siasa kukemea wafuasi wake waepukane na vitendo vya uvunjifu wa amani na kuwahamasisha kushindana kwa hoja.

“Tunasihi ushirikiano wa vyaka vyote vya siasa kutanguliza uzalendo wa nchi yetu kwanza na masilahi mapana ya Taifa letu, sote kwa pamoja tukemee na kuhamasiha wafuasi wetu kuondokana na vitendo vyote vyenye kuashiria uvunjaji wa amani,” amesema Askofu Sosthenes.

Askofu Sothenes amesema “ugomvi, matusi na kejeli hayo yote sio utamaduni wetu, tuendeleze utamaduni wetu wa kushindana kwa hoja, tunasisitiza na kuvisihi vyama vya siasa kuhimiza Watanzania pasipokujali itikadi zetu tufahamu Tanzania yetu inathamani zaidi kuliko tofauti zetu.”

 

Mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, ubunge, uwakilishi na udiwani unaendelea nchini Tanzania, ambapo kwa sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kutoa fomu za kugombea nafasi hizo.

Mchakato wa uchukuaji na urudishaji fomu unatarajia kumalizika tarehe 25 Agosti 2020, ukifuatia na zoezi la uteuzi wa wagombea, kisha kampeni zitaanza tarehe 26 Agosti mwaka huu, na kuhitimishwa tarehe 27 Oktoba 2020.

error: Content is protected !!