September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Viongozi wa dini wahimiza haki

Askofu Frederick Shoo, Mkuu wa Kanisa la KKKT

Spread the love

 

VIONGOZI wa dini kutoka madhehebu mbalimbali nchini Tanzania, wamehimiza Watanzania kuwa walinzi wa haki za binadamu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro…(endelea).

Wito huo umetolewa jana Jumatatu, tarehe 6 Desemba 2021, katika semina ya kuwajengea uwezo viongozi wa dini katika kushiriki kwenye utatuzi wa changamoto za kijami.

Iliyoandaliwa ba Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kwa kushirikiana na  Kamati ya Viongozi wa Dini inayohusu Haki za Kijamii na Uadilifu wa Uumbaji (ISCEJIC), inayoundwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).

Amifungua semina hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Askofu Fredrick Shoo,  ametoa wito kwa viongozi wa dini na Watanzania kwa ujumla kuhakikisha haki inatendeka kwa kuwa ndiyo tunda la amani.

“Viongozi wa dini ni wadau wakubwa wa maendeleo katika nchi yetu, kupitia taasisi zetu tunaendesha sehemu kubwa ya utoaji wa huduma za jamii hapa nchini, hii sio siri sisi ni wadau wakubwa maendeleo ya nchi hii. Taasisi za dini ni walezi wa jamii kupitia Imani na mafundisho ya Imani ambayo msingi wake ni ulinzi na uendelezaji wa utu wa mtu,” amesema  Askofu Shoo na kuongeza:

“Kuna kipindi kutaja swala haki ilikuwa ni jambo gumu. Sisi wenyewe tuwe Watetezi wa haki, tuzingatie haki za msingi za kila mwanadamu, ni kama ibilisi amefunga midomo ya watanzania tusitaje neno haki, tunataja upendo na Amani peke yake lakini tunahitaji kuongeza haki kwa sababu haki, ni jambo la msingi, pasipo haki hakuna Amani, Amani ni Tunda la Haki.”

Kwa Upande wake Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Sheikh Shaban Mlewa,  ametoa wito kwa viongozi mbalimbali, kuongoza kwa haki na upendo.

“Ni vyema tukajua wajibu wetu wa sasa ni kuijenga jamii na kuikumbusha kuzingatia haki, ni wajibu wa kila kiongozi kuwa na huruma, kuwa na Imani thabiti, kuonyesha upendo na haki yenyewe ambayo ndio msingi wa yote hayo,” amesema Sheikh Mlewa na kuongeza:

“Kusema kunaweza kusikilizwa na yoyote, lakini utendaji unaweza ukafuatiliwa na wengi, tunaweza kusema lakini tukafuatiliwa tunatenda kama tunavyoamrisha?, mara nyingi tuhamasishe tunayotenda ikiwemo kutenda haki ambayo ni wajibu wetu.”

Naye  mtoa mada katika mkutano huo,  ambaye ni Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, amepongeza hatua ya viongozi wa dini kuona umuhimu wa kujadiliana na kuongeza ujuzi katika uzingatiaji wa masuala  ya haki ambayo ni msingi wa amani na upendo kwa jamii.

“Dini na maswala ya haki za binadamu ni sawa na pande mbili za shilingi, haviwezi kuachana, ni vitu ambavyo vinakwenda pamoja ni vitu ambavyo vikikaa vizuri na kuelewana vizuri tunaamini tutakuwa na jamii ambayo inaheshimu na kulinda haki za binadamu , na ndio maana leo tumekuja kuwakumbusha kuwa wao ni walinzi namba moja wa haki za  binadamu kwa sababu ndio wanaohubiri maswala ya Upendo, Amani katika familia zetu,” amesema Olengurumwa na kuongeza:

“Na ulinzi wa haki za  binadamu unaanzia katika familia, Ulinzi wa haki za binadamu unaanzia kwa mtu mmoja mmoja, unakuja kwa familia, kaya, taifa na duniani kote, kwa hiyo viongozi wa dini wana nafasi kubwa na wanasikilizwa na watu wanawaelewa hivyo sisi tunawaona viognozi wa kidini kama watu wa muhimu sana katika ulinzi na utetezi wa haki za binadamu nchini na ni muhimu kushirikiana nao.”

error: Content is protected !!