August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Viongozi wa dini ‘wahifadhi’ aibu ya Tulia

Spread the love

“TUMERIDHIA ombi la viongozi wa dini,” ndivyo anavyosema James Mbatia, kwa niaba ya vyama vya upinzani vyenye wawakilishi bungeni na ambavyo vilikuwa katika mgomo wa kuhudhuria vikao vyote vya Bunge kila vinapoongozwa na Tulia Ackson, Naibu Spika wa bunge hilo, anaandika Pendo Omary.

Chama cha ACT Wazalendo, Chama cha wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na chama cha NCCR- Mageuzi ndivyo vyama pekee vya upinzani vyenye wawakilishi bungeni kati ya vyama 21 vya upinzani hapa nchini.

Vyama hivi, viliketi kwa muda wa siku mbili mfululizo kuzungumza na viongozi wa dini juu ya msimamo wao wa kususia vikao vyote vya Bunge vinavyoongozwa na Tulia kwa madai kuwa, kiongozi huyo amekuwa akiliendesha Bunge kibabe na kuwakandamiza wapinzani.

James Mbatia, Mbunge wa Jimbo la Vunjo na Mwenyekiti wa chama cha NCCR- Mageuzi amesema, “Tumefikia uamuzi wa kurejea bungeni baada ya kukubali ombi la viongozi wa dini tuliokutana nao kwenye kikao cha siku mbili,  kilichofanyika jana na  juzi.”

“Tumewaeleza viongozi wa dini sababu ya sisi kutoka bungeni ya kwamba, inatokana na Naibu Spika kutokuwa mzelendo na kutoweka  mbele maslahi ya taifa, huku akitukandamiza na kukitetea chama chake,” ameongeza Mbatia.

Mbatia pia, amelitaka Jeshi la Polisi hapa nchini, kuacha kutumika kisiasa  na kuingiza mambo ya jeshi hilo na siasa za kukibeba chama tawala huku likivikandamiza vyama vya upinzani.

“Hatua ya Jeshi la Polisi kuyahusisha mauaji ya polisi wanne yaliyotokea huko Mbagala Jijini hapa na harakati za siasa nchini ni hatua ya kuliaibisha jeshi hilo na kuchangia kuleta hofu kwa jamii. Ni vyema polisi wakaacha kutumika,” amesisitiza.

Kwa upande wake Ado Shaibu, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa ACT-Wazalendo, amemtaka Rais John Magufuli kupeleka muswaada bungeni ili kuvifuta vyama vya siasa vya upinzani na kubakisha CCM badala ya kutaka kusigina haki za vyama kufanya siasa.

“Hatua ya rais kuvikandamiza vyama vya upinzani haivumiliki na tutapambana kwa nguvu zote kuhakikisha, haki yetu ya msingi ya kufanya siasa inaheshimiwa na kulindwa,” amesema Ado huku akidokeza kuwa, chama chake kinasubiri barua kutoka Chadema ili nacho kijiunge na Oparesheni ya Kupinga Udiktea nchini (Ukuta).

 

error: Content is protected !!