October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Viongozi wa dini Mwanza wataka sheria kali kuwalinda Albino

Spread the love

 

KAMATI ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza, imeiomba Serikali iweke sheria kali na sera za kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyofanywa na baadhi ya watu kwa sababu ya imani za kishirikina. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Wito huo umetolewa hivi karibuni na wenyeviti wa kamati hiyo, Askofu Charlea Sekelwa na Sheikh Hassan Kabeke.

“Tunaiomba Serikali iboreshe na kusimamia sheria zinazowalinda watu wenye ualbino. Sheria hizi ziwe madhubutu kiasi kwamba wanapotendewa ukatili wahusika waadhibiwe vikali,” imesema tamko la kamati hiyo.

Wakati huo huo, kamati hiyo imeiomba Serikali kutengeneza sera rafiki zitakazowapa vipaumbele  watu wenye ualbino, ikiwemo kina mama na watoto wenye ualbino katika fursa za kielimu, ajira na mitaji ya ujasiriamali.

“Tunaiomba Serikali ipitishe rasimu ya mwongozo wa utoaji huduma za elimu kwa watu wenye ualbino Tanzania, kupitishwa rasimi hii kutasaidia kuwatengenezea wanafunzi wenye ualbino mazingira jumuishi ya kielimu shuleni,” imesema tamko la kamati hiyo.

Katika hatua nyingine, kamati hiyo imewaomba wananchi kuripoti matukio ya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watu wenye ualbino, katika vyombo vya dola ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Pia, imezitaka taasisi za dini nchini kutoa mafundisho na elimu kwa jamii, kutoka katika vitabu vitakatifu vya dini, namna Mungu anavyokemea ubaguzi.

error: Content is protected !!