Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Viongozi Tanga watakiwa kuwa wabunifu
Habari Mchanganyiko

Viongozi Tanga watakiwa kuwa wabunifu

Spread the love

VIONGOZI na watendaji wakuu wa halmashauri ya Jiji la Tanga wametakiwa kuwa wabunifu katika kuhakikisha wanawafikia wanawake wengi wanaoishi mjini ili waweze kujiunga na huduma za uzazi wa mpango. Anaripoti Khalifa Abdallah …. (endelea).

Wito huo umetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akifungua mkutano uliowakutanisha Viongozi na watendaji wakuu wa Halmashauri ya Jiji, Wilaya ya Tanga Mjini pamoja na Wilaya ya korogwe wenye lengo la kuendeleza juhudi za uzazi wa mpango nchini.

Waziri Ummy amesema kwamba Serikali ya awamu ya tano imejipanga kutokomeza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga hivyo imejipanga kuwafikia wananchi wengi ili kuweza kupunguza kwa asilimia 30 vifo vitokanavyo na uzazi.

“Lazima muonyeshe utayari na umakini kama viongozi katika kuwekeza kwenye uzazi wa mpango, mkiwa wabunifu mtawawezesha kuwafikia akina mama wengi wa mjini, hata akina baba kwa kuwapa elimu ya kutosha na kufanya maamuzi ili wapange lini wanataka kuzaa,watoto wangapi na watofautiane kwa miaka mingapi,” amesema Waziri Ummy.

Aidha, aliwataka viongozi kutumia fedha hizo kuziweka kwenye vitu endelevu ili mradi huo uongeze wanawake wengi kutumia njia za uzazi nchini.

“Msiweke mipango ya mardi huu kwenye semina bali mradi huu uwe njia ya kufungua miradi mingine kutoka kwa wadau wa maendeleo,” amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa Serikali kupitia Wizara ya afya kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019 umetenga Sh. 14 bilioni kwa ajili ya afya ya uzazi wa mama na mtoto tofauti na miaka ya nyuma ambapo kabla Serikali ya awamu ya tano haijaingia madarakani wizara ilikua ikitenga Sh. 2 bilioni kwa ajili ya matumizi kitengo hicho.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kisa Kasongwe ambaye alimuakilisha Mkuu wa Mkoa wa Jiji la Tanga alisema halmashauri ya Jiji la Tanga ipo tayari kutoa ushirikiano na shirika hilo kwani mradi huo utaleta hali nzuri kwa akina mama pamoja na watoto wachanga.

Wakati huo huo Kaimu Mwakilishi Mkazi wa shirika la jhpiego Dk. Dustan Bishanga alisema kuwa mradi huo unakuja kuongeza rasiliamali ambazo hazitoshi katika kusimamia na kutekeleza katika uwekezaji wa uzazi wa mpango.

“Mradi huu utafanikiwa endapo viongozi wa Jiji la Tanga mtatekeleza na kufanya mpango huu kufanikiwa hivyo mtapelekea tuwaletee mradi mwingine wa afya ya uzazi kwa vijana endapo mradi huu wa kwanza mtaufanikisha ipasavyo,” amesema Dk. Bishanga.

Mradi wa “Tupange pamoja” ulianzishwa mwaka 2016 na kutekelezwa na halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Arusha ambapo kwa jiji la Dar es Salaam walipatiwa shilingi milioni 250 kwa ajili ya kutekeleza uzazi wa mpango kwa halmashauri zote na hivi sasa unaanza kwa Jiji la Tanga.

Idadi ya akina mama wanaotumia uzazi wa mpango kwa Jiji la Tanga ni asilimia 31 ambapo kitaifa inatakiwa kufikia asilimia 45 hadi mwaka 2020 na vifo vya akina mama kwa halmashauri hii imepungua kutoka vifo 69 mwaka 2014 hadi vifo 45 kwa mwaka 2017.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Puma Energy Tz: Watanzania tudumishe amani kuvutia uwekezaji

Spread the loveKAMPUNI ya Mafuta ya Puma Tanzania imewakutanisha wadau mbalimbali katika...

Habari Mchanganyiko

DAWASA waanza utekelezaji agizo la Samia

Spread the loveMamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam...

Habari MchanganyikoKimataifa

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the loveTUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais wa...

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

error: Content is protected !!