July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Viongozi Halmashauri Sengerema kikaangoni

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wakazi wa Sengerema katika ziara yake ya siku tatu mkoani Mwanza

Spread the love

 

VIONGOZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, wako kikaangoni baada ya Serikali kutuma wakaguzi maalum, kukagua hesabu za halmashauri hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatatu, tarehe 14 Juni 2021 na Rais Samia Suluhu Hassan, katika ziara yake mkoani Mwanza.

Baada ya Mbunge wa Sengerema (CCM), Hamis Mwagao ‘Tabasamu’, kuiomba Serikali ilipe deni la bili ya umeme kiasi cha Sh. 300 milioni, inayodaiwa halamshauri hiyo na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), katika Mradi wa Maji wa Nyamazugo, unaogharimu Sh. 23 bilioni.

Bada ya Tabasamu kutoa ombi hilo, Rais Samia amesema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema inafuja fedha za Serikali, huku ikishindwa kukusanya mapato yake yenyewe.

“Halmashauri ya Sengerema haiko vizuri kwenye matumizi ya fedha, yenyewe haikusanyi fedha za kutosha lakini inafuja zinazoletwa. Serikali tumeamua kuleta wakaguzi maalum, kuangalia hesabu za halamshauri,” amesema Rais Samia.

Akizungumzia deni hilo, Rais Samia amesema inashangaza kuona halmashauri hiyo inadaiwa, wakati wananchi wanalipa bili za maji.

“Kuna madeni halmashauri inadaiwa, inashangaza kuona wananchi wanakosa maji sababu Wakala wa Maji Sengerema inadaiwa bili za umeme. Sasa sioni mantiki kama wananchi wanalipa, kwa nini washindwe kulipa na wao bili za umeme, maji yapatikane?” Amesema Rais Samia na kuongeza:

“Hii inaonesha Sengerema bado kuna kazi kubwa ifanyike, kwenye nyanja ya uongozi wa wilaya na halmashauri zake.”

Mbali na changamoto ya mradi huo, Tabasamu alimuomba Rais Samia aingilie kati mradi wa maji Igalula, ambao mkandarasi wake ameingia mikitini baada ya kupewa Sh. 460 milioni.

“Tunayo miraidi mikubwa ya maji, hii miradi ya maji amekuja Waziri wa Maji , Jumaa Aweso kuja kusimamia na kuangalia lakini njia zetu hazipitiki, hakupita kwenye mradi wa Igalula Sh. 4.6 bilioni, mkandarasi kapewa Sh. 460 milioni, hayupo site toka mwaka jana,” amesema Tabasamu.

error: Content is protected !!