September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Viongozi Chadema wazuiwa kwenda nje ya nchi

John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimelalamikia hatua ya viongozi wake tisa kuwekewa vikwazo vya kusafiri nje ya nchi, na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kufuatia Kesi ya Jinai Na. 112/2018 inayowakabili mahakamani hapo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Malalamiko hayo yametolewa na John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema, wakati akizungumza na wanahabari leo tarehe 7 Februari 2020, jijini Dar es Salaam.

Mrema amedai mahakama hiyo inawanyima ruhusa viongozi wa Chadema kinyume na Katiba ya Nchi, Ibara ya 17 A , kifungu cha 2B.

 “Nitaanza na safari ya terehe 13  hadi 17 Januari 2020 ambayo viongozi wakuu pamoja na wajumbe wa kamati kuu, walikuwa na safari ya kwenda nchini Kenya kwa ajili ya kukutana na kuweka mipango ya kuanza mwaka wa uchaguzi wa 2020.

Mawakili wetu waliandika barua kama ilivyo utaratibu wa mahakama, lakini hakimu akawazuia kwa hoja ya kwamba anataka na viongozi wakawe pale mahakamani,” amedai Mrema.

Mrema amedai masharti yaliyowekwa na mahakama hiyo, ikiwemo kuanzisha kesi mpya kuhusu maombi ya ruhusa ya kusafiri nje ya nchi, ni kinyume na katiba pamoja na sheria za nchi.

“Jambo ambalo ni la ajabu kabisa, sababu mwenye haki ya kutoa ruhusa ni mahakama, lakini leo viongozi wetu wakiomba ruhusa mahakama inaanzisha  kesi ndani ya kesi. Na hiyo kesi iwe na upande wa waomba ruhusa, serikali na mahakama,” amedai Mrema na kuongeza:

“Kitu ambacho si cha kawaida kwa washtakiwa wote, unachotakiwa kufanya ni kuieleza mahakama unaenda wapi, unapeleka na barua ya wadhamini kuthibitisha kwamba siku ya kesi utakuwa mahakamani. Ndio utaratibu lakini kwa viongozi wa chama utaratibu huo umekataliwa.”

Mrema amedai kuwa, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa ni mhanga mkuu wa changamoto hiyo,  licha ya kukubali sharti la mahakama hiyo kuanzisha kesi juu ya maombi ya ruhusa.

Mrema amedai baada ya Mbowe kuwasilisha maombi ya ruhusa hiyo, mawakili upande wa jamhuri  walifanya vitendo vilivyokwamisha kesi hiyo kusikilizwa kwa wakati.

“Hakimu Simba akishirikiana na mawakaili wa serikali wanazuia kumpatia kibali, alionyesha viza, tiketi za ndege za kwenda na kurudi na masuala ya ahadi ya biashara yalikuwa yameshakamilika. Mawakili wa serikali tangu tarehe 28 Januari kila siku wanakwepa.

  juzi wakavunja rekodi, Wakili wa Serikali, Nchimbi alisema hayuko Dar es Salaam yuko Kibaha, mawakili wetu wakafanya jitihada sababu tulipewa taarifa yuko ofisini kwake. Wakaenda, wakamkuta yuko ofisini kwake Dar es Salaam. Lakini mahakama anaidanganya yuko nje,” amedai Mrema.

Mrema amedai “Mawakili wa serikali wakakubalina na mahakama kwamba mwenye haki ya kwenda na kesi ni Wakili Faraja Nchimbi tofauti na utaratibu kwamba, mawakili wa serikali wanawakilisha kama mmoja hayupo.

Mawakili wa serikali wakaja na kisingizio kingine wanataka kuona passport yake, kwa sababu alikua tayari Dodoma akatuma nakala ambazo zilikuwa zimethibitishwa na mawakili kama ni halali. Ilitumwa jana wakapokea wakasema  uamuzi utafanyika leo asubuhi, mawakili wakaenda mahakamani wakaibuka na kitu kingine.”

Mrema amedai kitendo cha viongozi wake kuzuiwa kusafiri nje ya nchi , ni jambo la hatari kwa kuwa itafika mahali wananchi watakosa imani na mahakama.

“ Sasa mahakama inafika mahali inaachia uhuru wake, inakabidhi mawakili wa serikali.  Jambo la hatari kwa usalama wa nchi.  Inapofika mahali watu wanakosa imani na mhakama, kwamba wakienda polisi, serikalini, na bungeni hawapati haki, mahakama ndiyo inayobaki kutoa haki. Leo mahakama inakabidhi haki kwa serikali kupitia mawakili wa serikali kinyume na katiba,” amedai Mrema.

Mrema amesema Mbowe alikuwa na safari ya kwenda nchini Uingereza, Marekani na Uswiswi kuanzia tarehe 2 Februari , ambapo alipanga kurejea nchini tarehe 13 Februari mwaka huu.

Lakini kutokana na changamoto zilizojitokeza, ameamua kuondoa mahakamani hapo ombi la kupewa ruhusa, na hivyo anaendelea na vikao vya bunge vinavyoendelea jijini Dodoma.

Viongozi wengine wanaosthakiwa katika kesi hiyo ni pamoja na, John Mnyika, Katibu Mkuu Chadema,  Salum Mwalimu, Naibu Katibu Chadema Zanzibar , Esther Matiko, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, Mchungaji Peter Msigwa, Mwenyekiti Chadema Kanda ya Nyasa. Halima Mdee, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha).

error: Content is protected !!