KLABU ya Al-Nassr inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia imesitisha mkataba wa mshambuliaji wa Cameroon, Vincent Aboubakar ili kumpisha straika mpya raia wa Ureno, Cristiano Ronaldo. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa …(endelea).
Kwa mujibu wa kanuni za ligi hiyo, klabu zinaruhusiwa kuwa na wachezaji wanane wasio raia wa Saudi Arabia.
Kabla ya ujio wa Ronaldo, Al-Nassr ilikuwa imefikisha idadi ya wachezaji wanaoruhusiwa kwa hivyo ilikuwa lazima mmoja wao angetimuliwa ili kutengeneza nafasi ya nyota huyo wa Ureno.
Kwa mujibu wa RMC Sport, mkataba wa Aboubakar ulivunjwa baada ya makubaliano ya pamoja na atapokea malipo ya mkataba huo. Sasa ni mchezaji huru.
Aboubakar amehusishwa na uhamisho kuelekea klabu ya Manchester United ambayo inazidi kuwinda mshambuliaji katika dirisha fupi la uhamisho.
Raia huyo wa Cameroon alitamba katika Kombe la Dunia akifunga bao la ushindi dhidi ya Brazil. Pia alifunga mabao 13 na kutoa pasi 6 za mabao katika mechi 39 akiwa na miamba ya Al-Nassr.
Kuondoka kwa nahodha huyo wa Cameroon kunaruhusu Ronaldo kuandikishwa na kuwa huru kuchezea klabu yake mpya – japo atasubiri zaidi kwani anatumikia marufuku ya mechi mbili aliyopigwa kwa kuvunja simu ya shabiki akiwa nchini Uingereza.
Ronaldo tayari alikosa mechi ya kwanza ambako Al-Nassr iliipiga Al-Ta’ee 2-0 akitazama katika eneo la wageni mashuhuri na pia atakosa mechi ya Jumamosi ijayo dhidi ya Al-Shabab. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester United, Real Madrid na Juventus atakuwa huru kuchezea Al-Nassr tarehe 22 Januari, 2023 katika mechi yao ya nyumbani na Ettifaq.
Leave a comment