July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vinane vyaifuata CUF kususia uchaguzi

Spread the love

VYAMA vinane vilivyoshirikiki uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba mwaka jana vimetangaza kuwa havitoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu,Anaandika Faki Sosi.

Wawakilishi wa vyama hivyo wamesema msimamo wao ni kwamba uchaguzi mkuu wa Zanzibar ulifanyika 25 Oktoba 2015 na kilichotokea siku tatu baadaye ni kinyume cha Sheria ya Uchaguzi Zanzibar, Na. 11 ya mwaka 1984.

Vyama vilivyotangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio mbele ya waandishi wa habari walipokutana Hoteli ya Lambada, Ilala, Dar es Salaam ni Chauma, Demokrasia Makini, DP, Sau, Jahazi Asilia, NRA, UPDP na UMD.

Wawakilishi wao wamesema uchaguzi wa 25 Oktoba haujafutika kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na kwamba vyama hivyo vimesikitishwa na hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha ya kwenda kinyume na Katiba ya nchi.

Kwa mujibu wa maelezo yao, Jecha amefanya kosa la uhaini kwenye nchi ya kidemokrasia na anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Vyama hivyo vimewakilishwa na Ali Omari Juma (Katibu Mkuu Chauma), Mohamed Masoud Rashid (Makamo Mwenyekiti wa Chauma ambaye aligombea urais), Abdalla Kombo Khamis (mgombea urais Zanzibar kupita Democratic Party (DP), Tabu Mussa Juma (Demokrasia Makini ambaye alikuwa mgombea urais), Kassim Bakar Ali (Mwenyekiti Jahazi Asilia ambaye alikuwa mgombea urais).

Wengine ni Aziz Mohamed Ali (Naibu Katibu Mkuu Sau), Suleimani Said Mohammed (Naibu Katibu Mkuu UMD) na Suleiman Mohamed Gaddafi (Naibu Katibu Mkuu NRA).

Baadhi ya vyama pia viliandamana na waliokuwa wagombea urais katika uchaguzi uliofutwa kibabe. NRA ilikuwa na Seif Ali Idd.

Kiongozi wa Chauma, Mohamed Masoud Rashid, akiwakilisha wawakilishi wa vyama hivyo amesema tarehe 6 Februari 2016 walikutana na baada ya majadiliano walikubaliana vyama vyao visishiriki uchaguzi wa marudio kwa kuwa si halali kwa kuwa uchaguzi uliofutwa ulikuwa halali kisheria.

Alisema wamefikia uamuzi huo kwa hiyari yao na haitokani na kushawishiwa na mtu au chama chochote cha siasa, bali wameguswa na maslahi ya wananchi na kulinda Katiba ya Zanzibar.

Amesema wanahofu kwamba uchaguzi ulioitishwa isivyo halali hautakuwa halali na badala yake utakumbwa na vurugu na umwagaji wa damu, wizi wa kura na hivyo kuchochea amani kuvunjika kutokana na matumizi makubwa ya vikosi vya jeshi vilivyoandaliwa.

Akinukuu vifungu vya sheria, Masoud amesema Jecha amefuta uchaguzi kwa utashi wake kwani amekiuka tafsiri ya vifungu 19, 20, 21(1), (a), (b), (c), (d), (2) na 22 vya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ya 1984.

Masoud amesema Rais John Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hawezi kuliepuka suala la Zanzibar na akikataa kujihusisha nalo atawagawa Watanzania.

Amesema aliyoyasema kwamba hana mamlaka ya kuingilia kwa kudai tume ni huru kama zilivyo tume za nchi nyingine, ni kauli ya utashi wake binafsi unaotokana na kuzingatia maslahi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ali Omar Juma, Katibu Mkuu wa Chauma amesema amesikitishwa na kauli ya Rais Magufuli ya kukwepa jukumu muhimu la kikatiba wakati yeye ndio Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya ulinzi na usalama katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Omar amesema iwapo msimamo huo ni sahihi, basi Rais Magufuli hapaswi kupeleka majeshi Zanzibar katika kipindi cha maandalizi ya uchaguzi wa marudio, vinginevyo amethibitisha Zanzibar haina haki ndani ya Muungano.

Wawakilishi wa vyama hivyo wamethibitisha msimamo wao kwa kumuandikia rasmi Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar, Salum Kassim Ali, ambaye alivitaka vyama vyote kueleza msimamo wao kufikia 12 Februari.

Tayari Chama cha Wananchi (CUF) kilishatangaza mapema kutoshiriki uchaguzi wa marudio kwa msimamo kuwa uchaguzi ulishafanyika 25 Oktoba na kusifiwa kuwa ulikidhi vigezo vya kisheria.

error: Content is protected !!