August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vilio, simanzi maafa ya watoto wanne

Spread the love

WATOTO wanne wa familia moja wameteketea kwa moto uliotokana na kulipuka kwa kibatari wakati wa usiku wa kuamkina jana, anaandika Dany Tibason.

Msimamizi wa familia hiyo Rameki Mdachi amesema kuwa, mauti yaliwafika watoto hao kati ya saa tano na nusu na saa sita usiku kutokana na kibatari kulipuka na kuaza kuungiza godoro na chandarua.

Amesema, moto huo ulipamba moto zaidi baada ya kuanza kuunguza chandarua pamoja na godoro na kwamba, moshi mkali uliwafanya watoto hao ulisababisha kuwakosesha nguvu na hatimaye kufariki kabla ya kuokolewa.

Msimamizi huyo wa familia amesema kuwa, baba mzazi wa watoto waliofariki tayari alifariki siku za nyuma hivyo watoto hao walikuwa wakilelewa na mama yao aliyemtaja kwa jina la Roda Mdachi ambaye ni mjane na kuwa, alikuwa shambani kwake Ngese, Kiteto wilayani Manyara.

Rameck amesema, wakati mama yao na watoto hao akiwa shambani, alimwacha msichana ambaye hakumtaja jina na kueleza kuwa;

“Inaonesha dada huyo aliwaacha watoto hao na kuwafungia ndani huku wakiwa wamewasha kibatari ambacho kililipuka na kusababisha kuunguza godoro na kibatari na kusababisha mauti kwa watoto hao,” amesema.

Watoto waliofariki katika tukio hilo walitambuliwa kwa jina la Samwel Mdachi (7), darasa la kwanza, Elizabeth Ndachi (11) darasa la sita, Nasse Mgaba (9) darasa la tatu wote wanafunzi wa Shule ya Msingi Miembeni huku Peter Lema (9) akiwa mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi St. Poul iliyopo katika Mji Mdogo wa Kibaigwa.

Ramekin amesema, katika watoto waliokufa, watoto wawili ni ndugu huku watoto wawili wakiwa ni wajukuu wa mama mjane ambaye alifiwa na mume wake miaka mitatu iliyopita.

Mashuhuda waliokuwepo katika tukio hilo lililotokea katika Mtaa wa Nyerere katika Wilaya ya Kongwa Mji Mdogo wa Kibaigwa mkoani Dodoma wamesema, moto huo uliosababisha vifo vya watoto hao ulitokea majira kati ya saa tano nusu usiku na saa sita.

Mmoja wa mashuhuda katika tukio hilo ambaye ni mchungaji wa kanisa la kusudi kuu la Mungu, Dickson Muhina, amesema majira ya saa tano na nusu usiku mke wake alisikia kelele kwa majirani baada ya kutokea kwa moto huo.

Amesema, baada ya kutoka ndani kwake aliona wingu zito la moshi ambalo lilikuwa likitokea katika nyumba hiyo jambo ambalo alishirikiana na majirani kuwavunja milango na madirisha kwa lengo la kuoka watoto watoto hao lakini juhudi ziligonga mwamba.

Kwa upande wake mganga wa Wilaya ya Kongwa, Dk. Anisenta Munishi, alithibitisha kuwepo kwa vifo hivyo ambavyo amesema vimesababishwa moto uliotokana na kulipuka kwa kibatari.

Amesema, kutokana na nyumba hiyo kutokuwa na madirisha mapana nay a kuingiza hewa ya kutosha watoto hao walianza kufa kwa moshi na baadaye moto uliwamalizia.

Kwa upande wao wananchi wakizungumzia tukio hilo wamesema, sababu kubwa ya kulipuka kwa vibatari ni kutokana na mafuta ya taa kuchanganywa na Petrol.

Akizungumzia kuchanganywa kwa mafuta Machite Mugurambwa, amesema kumekuwepo na wauzaji wa mafuta kuchanganya mafuta ya taa na yale ya petrol.

“Matukio ya kulipuka kwa vibatari, yamekuwa makubwa sana hapa Kibaigwa lakini inatokana na wale wanaouza mafuta ya rejareja kutumia dumu moja kununulia mafuta ama wakati mwingine kuchanganya mafuta ya taa na petrol.

“Hilo kama halitoshi hapa Kibaigwa hakuna gari la zima moto hivyo ni lazima kuagiza zimamoto kutoka mkoani Dodoma jambo ambalo linasababisha kuwepo kwa vifo vingi ambavyo vinatokana na moto.

“Mji mdogo wa Kibaigwa unatakiwa kuwa na gari la zima moto hivyo ni wito wangu kwa serikali kuhakikisha wanaweka gari la zima moto ili kuepusha vifo ambavyo ninatokea kutokana na moto” amesema Machite.

 

error: Content is protected !!