June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vikwazo kibao biashara Afrika Mashariki

Spread the love

SERIKALI imekiri kuwa, kufanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki bado kuna changamoto na vikwazo visivyo vya kiforodha ambavyo hujitokeza kwa wafanyabiashara. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba ambaye amesema kuwa vikwazo hivyo hutokea kwa wafanyabiashara kinyume na makubaliano ya Afrika Mashariki.

Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Micheweni (CUF) Haji Khatib Kai ambaye alitaka kujua Serikali inawashauri nini wananchi wanaopenda kufanya biashara kwenye nchi zilizokatika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mbunge huyo alihoji kuwa ni wapi wananchi wanapopata matatizo katika biashara hizo wanaweza kupeleka malalamiko yao ili yafanyiwe kazi kwa wakati.

Naibu Waziri amesema nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeondoleana ushuru wa forodha mipakani, hatua ambayo inapanua soko la Tanzania kufika kwa wanajumuiya hiyo wanaokadiriwa kufikia 143 milioni.

Amesema endapo soko hilo linalounganisha nchi za Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi likitumika vema, litachangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa taifa na kupunguza umasikini wa wananchi.

“Kwanza serikali inawashauri wananchi kuzichangamkia fulsa za kibiashara, ajira na uwekezaji zitokanazo na jumuiya ya Afrika Mashariki katika kujihakikishia maendeleo na serikali inawashauri wananchi hao kuzitambua taratibu za kufuata katika kutumia fursa za biashara,” amesema Kolimba.

Katika majibu ya nyongeza, Waziri wa Katiba na Sheria Dk, Harrison Mwakyembe amesema kuwa Tanzania imekuwa ikitumia nafasi mbalimbali katika kuwapa elimu wananchi wake juu ya kuzitumia fulsa hizo kwa faida yao na taifa.

Aliwataka wananchi kutumia nafasi yao katika kutoa elimu kwa wananchi katika majimbo yao ili kuzingatia fursa za kibiashara, ajira, uwekezaji ambazo zipo katika jumuiya ya Afrika Mashariki.

error: Content is protected !!